Okwi afunguka usajili Salamba, Kaheza Simba

Thursday June 14 2018Mshambuliaji wa Simba Emmanuel Okwi.

Mshambuliaji wa Simba Emmanuel Okwi. 

By Eliya Solomon, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Mchezaji wa kimataifa wa Simba, Emmanuel Okwi amesema atashirikiana vyema na mshambuliaji yeyote mpya atakayepangwa kwenye kikosi cha kwanza.

Okwi aliyerejea kwao Uganda kwa mapumziko, alisema kazi yake ni kucheza mpira na hawezi kuchagua mshambuliaji wa kucheza naye ingawa msimu uliopita alifunga mabao 20 akifanya vizuri na nahodha wake John Bocco.

Bocco alishika nafasi ya pili kwa ufungaji akifunga mabao 14 katika michuano hiyo

“Naweza kusema nilifurahia sana kucheza na Bocco lakini kuna kipindi anaweza kupata majeraha au mimi naweza kuumia kwa hiyo kama wachezaji ni vyema kuwa na maelewano.

“Nikiwa na maelewano na kila mchezaji inamaana sitapata shida ya kucheza na yeyote, ni mapema mno kusema nina maelewano ya kucheza na wachezaji wapya,” alisema Mganda huyo.

Okwi alisema usajili wa Adam Salamba kutoka Lipuli, Mohammed Rashid (Prisons) na Marcel Kaheza (Majimaji) utaongeza ushindani.

Alisema hakuna mchezaji ambaye atabweteka kwa kuwa atalazimika kuongeza juhudi kuendelea kupata namba katika kikosi cha kwanza.

Simba imenasa saini za Salamba, Kaheza na Rashid baada ya wachezaji hao kucheza kwa kiwango bora katika michuano ya Ligi Kuu Tanzania Bara msimu uliopita. Simba ilitwaa ubingwa msimu huu.

Advertisement