Partey amnyanyua kwapa Arteta

Muktasari:

Kiwango cha Partey kilionekana kuwa cha kawaida tu kwenye usiku huo wa Arsenal huko Austria, huku mabao ya David Luiz na Pierre-Emerick Aubameyang yakiwabeba na kushinda 2-1 baada ya kipa Bernd Leno makosa yake kuwazawaidia bao la kuongoza wenyewe kwenye kipindi cha pili.

London, England. Mikel Arteta amemwaga sifa kibao kwa kiungo wake mpya Thomas Partey kwa alichokifanya kwenye mchezo wa kwanza katika kikosi cha Arsenal aliocheza kwa dakika zote wakati miamba hiyo ya Emirates ilipotokea nyuma na kuichapa Rapid Vienna ugenini kwenye mikikimikiki ya Europa League.

Kocha Arteta amewatisha wapinzani wao kwamba Partey ndio kwanza anapasha misuli tu, mambo mengi matamu yatakuja.

Kiwango cha Partey kilionekana kuwa cha kawaida tu kwenye usiku huo wa Arsenal huko Austria, huku mabao ya David Luiz na Pierre-Emerick Aubameyang yakiwabeba na kushinda 2-1 baada ya kipa Bernd Leno makosa yake kuwazawaidia bao la kuongoza wenyewe kwenye kipindi cha pili.

Kiungo huyo wa kimataifa wa Ghana alikuwa kwenye rada za Arsenal kwa muda mrefu kabla ya kutoa mkwanja kunasa huduma ya mkali wao huyo wanayemsaka kutoka Atletico Madrid katika dakika za mwisho kabisa za kufungwa kwa dirisha la usajili. Alisema mechi yake ya kwanza ya Ligi Kuu England alipotokea benchi dhidi ya Manchester City, lakini alikuwa moto zaidi juzi usiku alipoanzishwa kwa mara ya kwanza.

“Kwa kusema ukweli alikuwa mwamba kwelikweli, alitulia sana,” alisema Arteta.

“Nadhani aliikamatia kiungo kwenye kipindi cha pili na alifungua uwanja na kuwafanya wachezaji wa ushambuliaji kuwa huru. Alikuwa bora usiku ule na nadhani mambo matamu yatakuja zaidi.”

Arsenal ilikuwa kweye kiwango kibovu katika kipindi cha kwanza na mambo yalionekana kuwa magumu baada ya Taxiarchis Fountas kuifungia Rapid bao la kuongeza kabla ya kufunga mara mbili ndani ya dakika nne, Luiz akiunganisha kwa kichwa krosi ya Nicolas Pepe na Aubameyang kupiga chuma cha pili akitokea benchi.

Wachezaji wanaokunja mishahara mikubwa kwa wiki huko Arsenal ni Aubameyang - Pauni 350,000, Ozil - Pauni 350,000, Willian - Pauni 220,000, Lacazette - 182,000, Pepe - 140,000, David Luiz - Pauni 125,000, Bellerin - Pauni 110,000, Kolasinac - Pauni 100,000, Bernd Leno - Pauni 100,000 na Xhaka - Pauni 100,000