Pluijm aitaka mikoba ya Amunike Stars

Dar es Salaam. Kocha wa zamani wa Yanga, Hans van der Pluijm amekimezea mate kibarua cha kuinoa timu ya taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ baada ya kutimuliwa kwa Emmanuel Amunike.

Amunike alitimuliwa siku chache zilizopita baada ya Taifa Stars kuondolewa mapema katika Fainali za Mataifa ya Afrika (Afcon) zinazoendelea kutimua vumbi nchini Misri.

Wakati ikielezwa tayari mchakato wa kumtafuta mrithi wa Amunike umeanza, Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), limemteua Etienne Ndayiragije kuwa kaimu kocha mkuu atakayesaidiwa na Juma Mgunda pamoja na Suleiman Matola kuionoa Stars kwa ajili ya michezo ya kuwania tiketi ya kufuzu michuano ya Fainali za Wachezaji wa Ndani ya Afrika (Chan), itakayopigwa Cameroon, mwakani.

Benchi hilo la ufundi la muda liliteuliwa baada ya kikao cha dharura cha kamati ya utendaji ya TFF.

Hata hivyo, hivi karibuni katibu mkuu wa TFF, Kidao Wilfred alisema makocha kadhaa wameanza kuwasilisha maombi ya kuinoa Taifa Stars, lakini hakuweka wazi majina yao.

“Wapo makocha kutoka Ulaya na wengine ni hapa hapa Afrika ambao tayari wameshatuma maombi. Tuiachie kamati ifanye kazi yake,” alisema Kidao ambaye katika mahojiano yaliyopita na gazeti hili alisema kati ya makocha hao wapo kutoka Hispania, Sweden na wengine Ulaya Mashariki.

Hata hivyo, akizungumza kutoka Ghana anakoishi, Pluijm alisema kwa njia ya simu kuwa anaitaka nafasi hiyo na ikionekana anafaa atakuwa tayari kurejea nchini kuchukua mikoba ya Mnigeria huyo.

Kocha huyo Mholanzi alisema ana uzoefu wa kutosha kutokana na kufundisha klabu kadhaa za Ligi Kuu Tanzania Bara kwa mafanikio ikiwemo Yanga, Azam na Singida United.

“Wenye maamuzi ni TFF, kama wakiona ninafaa basi naweza kuwa msaada wa kuivusha timu ya taifa ya Tanzania ilipo kupiga hatua zaidi, ni muda wa kujaribu kuwa na misingi ya mpira ambayo itakuwa ikiendelezwa,” alisema kocha huyo.

“Hakuna kitu kibaya kama kutokuwa na msingi, nachojua akiwepo hata kocha akiondoka basi ni lazima anayekuja aje na mipango itakayokuwa ikifuata misingi iliyopo.”

Klabu ya mwisho kwa Pluijm kuifundisha nchini kabla ya kurejea kwao ni Azam FC ambayo aliipa ubingwa wa Kombe la Mapinduzi.

Kocha huyo amekuwa akitumia mbinu za soka la kushambulia kwenye ufundishaji wake, huku akiwatumia viungo wakabaji wenye uwezo wa kusambaza mipira kwa haraka.