Pyramids inafungika dakika hizi

Dar es Salaam. Yanga inatarajiwa kuvaana na Pyramids ya Misri katika mchezo wa Kombe la Shirikisho Afrika kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.

Yanga na Pyramids zitacheza keshokutwa mchezo huo wa hatua ya mchujo na timu hizo zitarudiana Novemba 3 nchini Misri.

Yanga ambao ni mabingwa wa kihistoria wa Ligi Kuu wakiweka rekodi ya kutwaa ubingwa mara 27, wanaivaa Pyramids baada ya kuifunga Mbao bao 1-0 kwenye uwanja huo.

Akizungumza jana Kocha wa Yanga Mwinyi Zahera alisema ameifuatilia Pyramids licha ya kuwa ina uwezo mkubwa kiuchumi lakini ni dhaifu katika baadhi ya idara zake.

Zahera alisema moja ya mbinu aliyotumia kuwasoma wapinzani wake ni kuangalia baadhi ya mikanda ya video na kubaini haina ukuta imara.

‘Tumeona udhaifu wao tumeufanyia kazi tutacheza kwa umakini kwa kushambulia muda wote ili kupata matokeo mazuri,”alisema Zahera. Licha ya Pyramids kuundwa na kikosi cha gharama, lakini safu yake ya ulinzi imeonyesha udhaifu kwa kuruhusu idadi kubwa ya mabao kipindi cha pili.

Katika mechi 10 ilizocheza hivi karibuni za mashindano yote, Pyramids imefunga mabao 17, saba ikifunga kipindi cha kwanza na 10 kipindi cha pili.

Rekodi zinaonyesha imefungwa mabao tisa katika mechi 10 na yote kipindi cha pili, hivyo Yanga inaweza kutumia udhaifu huo kupata mabao endapo itacheza kwa nidhamu.

Mabao iliyofungwa kipindi cha pili dhidi ya wapinzani wake yamefungwa kuanzia dakika ya 50 hadi 90. Pyramids imeruhusu mabao mengi zaidi kuanzia dakika ya 60 hadi 90 kwani imefungwa manane katika dakika hizo.

Yanga katika michezo 10 iliyopita ya mashindano yote imeruhusu mabao matano kipindi cha kwanza na matano kipindi cha pili huku ikifunga matano kipindi cha kwanza na matano kipindi cha pili.

Pia Pyramids hawako nyuma katika kufunga mabao kwani imeonekana ni hatari kufunga mabao kipindi cha pili kuanzia dakika ya 48 hadi 80 kati ya mabao 10 iliyofunga katika mechi 10, tisa imefunga ndani ya dakika hizo.

Mchambuzi Ally Mayay alisema Yanga inatakiwa kuwasoma vizuri wapinzani wao na kwenda tofauti nao kama wanataka kufanya vizuri katika mchezo huo.

“Nakumbuka kipindi fulani cha Sir Alex Ferguson, Manchester United iliwahi kucheza mechi 15 ikawa inafunga kuanzia dakika ya 85 na kuendelea hivyo makocha wa timu pinzani walipogundua hilo waliamua kuanzia dakika hizo kufanya mabadiliko kwa kuwatoa washambuliaji na kuwaingiza viungo kwenda kuzuia kwasababu walikuwa wakijua jinsi Manchester inavyokuwa moto dakika hizo.

“Yanga inatakiwa kufanya hivyo kwa kuangalia kama kipindi cha pili Pyramids ndio huwa wanafunga zaidi inabidi wazuie kwani wapinzani wao watakuwa na akili hiyo hiyo ya kuingia uwanjani wakiamini kwamba muda fulani ndio tunafunga sana hivyo wanajipanga vizuri zaidi.

“Inavyoonekana kwenye maandalizi ya msimu kwa Yanga kuna vitu walivikosa kwa sababu ukiingalia mechi nyingi wanaanza kwa kasi kipindi cha kwanza lakini muda unavyosogea wanachoka.

“Hivyo Yanga ili kuitumia kasi yao vizuri kipindi cha kwanza waanzishwe wachezaji machachari kama Mrisho Ngassa, Mapinduzi Balama. Bora wakatumika mapema ili nguvu yao itumike kuzalisha mabao mapema na kipindi cha pili wanaweza kuingiza viungo wakabaji kama Tshishimbi, Makame, Fei Toto kwa ajili ya kuanza kulinda,” alisema Mayay.

Nyota wa zamani wa Yanga Sekilojo Chambua alisema wajiandae kucheza kwa umakini kwa kuwa wanacheza na timu ngumu. “Kipa lazima azungumze muda wote na mabeki wake kwani Pyrmaids wana washambuliaji wabunifu ambao muda wowote wanatumia nafasi na wanakufunga.

Mabeki wetu kwa kuzingatia tunacheza nyumbani wanatakiwa wacheze kwa umakini na washambuliaji watulie wanapofika langoni waongeze ubunifu na kutumia nafasi,” alisema Chambua.