Rashford ataja kikosi cha nyota sita Man Utd

Manchester, England. Mshambuliaji wa Manchester United, Marcus Rashford ametaja mastaa sita ambao hawawezi kukosekana katika kikosi cha United cha muda wote, iwapo angepewa nafasi ya kuwateua.

Katika kikosi chake, mchezaji huyo amewajumuisha Cristiano Ronaldo katika eneo la mbele, Wayne Rooney, Ryan Giggs na Paul Scholes.

Rashford alisema katika kikosi chake Ronaldo atacheza kama winga wa kushoto huku Giggs akishambulia kutokea kulia na katika eneo la katikati la ushambuliaji kutakuwa na Rooney ambaye amemsifia kuwa mshambuliaji bora aliyewahi kucheza naye kikosini kabla hajatimka.

Rashford (22) ambaye amefunga mabao 41 katika mechi 133 kwenye kikosi cha Mashetani Wekundu tangu atue 2015, alisema katika eneo la beki wa kati kutakuwa na Rio Ferdnand. “Pale akisimama Rio hakuna shaka kwamba wachezaji wengine wataucheza vizuri mpira, huku wakiisaidia timu kushambulia na kufunga bila wasiwasi,” alisema.

Ingawa Rashford, aliyefunga mabao 10 katika michezo 38 aliyoichezea England, alisema: “Labda pia ningekuwa na (David) De Gea, lakini bila shaka atasimama mzee mzima (Edwin) van der Sar ili tusifungwe.” Kuhusu yeye kutokuwa sehemu ya kikosi hicho, alisema, “nitakuwa nje, siwezi kutia mguu ndani (ya uwanja).”

Rashford alimtaja Rooney kuwa mchezaji bora aliyecheza naye akisema, “kupata nafasi ya kucheza naye ilikuwa jambo la kushangaza na ni vitu vidogo tu alivyotufanyia (kabla ya kuondoka United).”

Pia, aliwasifia Rooney na Giggs kwa kusaidia maendeleo yake kama mchezaji.

Alipoulizwa ni mchezaji gani aliyejifunza zaidi kutoka kwake kwa kifupi Rashford alijibu, “Rooney au labda Giggs wakati naingia kwanza alikuwa akifundisha (Louis) van Gaal. Yeye (Giggs) alinisaidia sana.”