Rekodi ya Mtibwa Sugar inavyohatarisha ubingwa wa Simba mechi zao mbili

Wednesday May 15 2019

 

By OLIPA ASSA

PAMOJA na Simba kupewa nafasi kubwa ya ubingwa, huku Yanga wakionekana njia yao nyembamba, Wanamsimbazi hao bado wana mtihani mgumu kwa baadhi ya mechi walizobakiwa nazo.

Yanga wamebakiza mechi mbili dhidi Mbeya City na Azam FC, wakifanikiwa kushinda zote watafikisha jumla ya pointi 89, lakini Simba wamebakiwa na mechi tano, wakishinda hizo watakuwa na pointi 97 watakuwa juu ya watani wao Wanajangwani kwa nane.

Licha ya Simba kupewa nafasi kubwa lakini sio kazi rahisi kwao kwani wamebakiza mechi ngumu dhidi ya Mtibwa Sugar (nyumbani na ugenini), Singida United, Ndanda FC na Biashara.

Mtibwa Sugar ni timu ambayo ina changamoto kwa klabu kongwe, tayari walishaifunga Yanga kwenye Uwanja wao wa Jamhuri, bao 1-0 na walipocheza Taifa walifungwa mabao 2-1.

Kocha wa Simba, Patrick Aussems baada ya kupoteza na Kagera Sugar, akiambulia pointi moja na Azam FC waliotoka nayo suluhu, aliapa kuanza kuvuna pointi dhidi ya Mtibwa Sugar.

"Nimeishajua changamoto za kutokufanya vyema katika mechi mbili dhidi ya Kagera na Azam FC, naamini mechi yetu na Mtibwa Sugar itaturudisha kwenye mstari wa ushindani na mwelekeo wa ubingwa kwani bado tuna nafasi kubwa.

Advertisement

"Mtibwa Sugar ni timu yenye ushindani wa hali ya juu, lakini wachezaji wangu nawaamini wapo tayari kwenda kupambania ubingwa"anasema.

Kocha wa Mtibwa Sugar, Zuber Katwila anasema wanaiheshimu Simba na kudai kwamba ataingiza kikosi chake uwanjani kwa ajili kuvuna pointi tatu.

"Malengo yetu kila tunapocheza mechi ni kuchukua pointi tatu kwa kila timu ambayo tutakayocheza nayo, tunajua Simba wapo vizuri na sisi tupo vizuri"anasema.

Advertisement