Shabiki afia Uwanjani Madagascar vs Senegal

Monday September 10 2018

 

Antananarivo, Madagascar. Shabiki mmoja wa soka amefariki Dunia na wengi karibu 40 kujeruhiwa kutokana na msongamano uliojitokeza wakati wa kuingia uwanjani kushuhudia mchezo kati ya Madagascar dhidi ya Senegal.

Pambano hilo lililofanyika kwenye Uwanja wa Municipal de Mahamasina mjini  Antananarivo, lilikuwa la kuwania kufuzu fainali za Afrika mwaka 2019 zitakazofanyika nchini Cameroon.

Kifo hicho kilitokea wakati maelfu ya watu walipojaribu kulazimisha kuingia uwanjani kwa kupimana ubavu na polisi.

Msemaji wa polisi alisema jana kuwa kati ya majeruhi waliopelekwa hospitali mjini Antananarivo, walikuwa kwenye hali mbaya.

Baadhi ya mashuhuda wa tukio hilo aliwatupia lawama wasimamizi wa uwanja huo wa Municipal de Mahamasina, kwa kufungua mlango mmoja pekee wakati wakijua huo ulikuwa mchezo mkubwa.

“Watu walilazimika kusukumana kwa sababu mlango uliofunguliwa ulikuwa mmoja na kila mtu alitaka kuwahi kuingia baada ya kununua tiketi yake,” alisema Rivo Raberisaona.

"Nadhani katika hili polisi wanawajibika kwa sababu waliona msongamano ulivyokuwa lakini wakashindwa kuwaamuru wasimamizi wa uwanja kufungua milango mingine, “ alisema Henintsoa Mialy Harizafy.

Imeelezwa kuwa watu walimiminika uwanjani kwa nia ya kuwaona mastaa wa Senegal akiwemo nyota wa klabu ya Liverpool, Sadio Mané, ambaye alicheza katika mechi hiyo iliyoisha kwa sare ya mabao 2-2.

Kumekuwa na matatizo sana kwa wasimamizi wa viwanja kushindwa kuwajali mashabiki barani Afrika, Februari mwaka 2017 mashabiki 17 walifariki Dunia nchini Angola na Julai mwaka huo mashabiki wanane wakiwemo watoto saba walifariki Dunia nchini Malawi.

Advertisement