Sheria za Lampard zaibua mjadala

Dar es Salaam. Sheria za kocha wa Chelsea, Frank Lampard katika kudhibiti nidhamu kwa nyota wake, zimewaibua makocha wa Ligi Kuu Bara.

Wakizungumza Dar es Salaam jana, makocha Mohamed ‘Adolf’ Richard, Abdallah Mohammed na Idd Nassor ‘Cheche’ walitoa maoni tofauti kuhusu udhibiti wa wa nidhamu kwa wachezaji nchini.

Rishard anayeinoa Prisons, Adolf alisema zipo adhabu kwa mujibu wa sheria ambazo mchezaji akikiuka anakatwa kulingana na kosa ingawa hakutaka kuweka wazi kiasi gani.

“Tunaweza kuwa na wachezaji makini nchini kama tutakuwa na sheria za namna hiyo hata kama bado soka letu linasafari ndefu viongozi wa klabu wanatakiwa kushirikiana na makocha kudhibiti utovu wa nidhamu kwa wachezaji.”

Kocha wa JKT Tanzania, Mohammed alisema. “Kuna mambo yanakera, mnaweza kukubalina kuanza mazoezi muda fulani lakini unakuta mchezaji anachelewa bila sababu ya msingi, tabia ya namna hiyo ni mbaya.”

Cheche ambaye ni kocha msaidizi wa Azam, alisema sheria hizo hapa nchini zitakuwa na tija endapo kutakuwa na mawasiliano baina ya viongozi na makocha.

Mwenyekiti wa bodi ya Wakurugenzi wa Simba ambaye ni mwekezaji wa timu hiyo, Mohammed Dewji naye ni kati ya waliovutiwa na sheria za Lampard.