Sibomana ang’ara, Mkwasa kicheko

Saturday November 9 2019

 

By Mwandishi Wetu, Mwananchi

Dar es Salaam. Bao la mchezaji wa kigeni Patrick Sibomana limembeba kocha Charles Mkwasa ambaye ameiongoza Yanga katika mchezo wake wa kwanza tangu alipoteuliwa kujaza nafasi ya Mwinyi Zahera.

Mkwasa aliyeteuliwa kuinoa Yanga kwa muda, ameanza vyema kazi yake baada ya kuipa timu hiyo ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Ndanda kwenye Uwanja wa Nangwanda Sijaona, Mtwara.

Muda mfupi baada ya kuteuliwa, Mkwasa aliahidi kurejesha furaha kwa mashabiki wa Yanga akianzia katika mchezo huo wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Katika mchezo wa jana, Mkwasa ambaye amewahi kuwa katibu mkuu wa klabu hiyo, alifanya mabadiliko katika kikosi kwa kuwapa nafasi Jafari Mohammed na Rafael Daud.

Jafari alicheza beki wa kulia badala ya Juma Abdul ambaye katika mechi zilizopita alikuwa akicheza. Pia Daud alicheza nafasi ya ushambuliaji namba 10. Kipindi cha pili Daud alitoka na kuingia Mrisho Ngassa.

Nahodha Papy Tshishimbi ambaye kwa asili ni mchezaji wa kiungo, alicheza katika nafasi hiyo tofauti na awali ambapo alikuwa akipangwa namba 10.

Advertisement

Mabadiliko mengine Mkwasa alimuanzisha winga Deus Kaseke ambaye amekuwa akitokea benchi lakini jana alianza katika mchezo huo.

Pia Ally Mtoni ‘Sonso’ aliyekuwa akicheza beki wa kushoto alicheza na Kelvin Yondani katika nafasi ya ulinzi wa kati. Yondani amekuwa akicheza na Lamine Moro.

Akizungumza jana, Mkwasa alisema ana furaha kupata ushindi ambao umetokana na kazi ngumu waliyofanya wachezaji wake.

“Nawapongeza wachezaji wamefanya vile tulivyopanga licha ya kwamba ni muda mfupi kuwa pamoja nao lakini wamepambana.

“Tulijaribu kuzuia na kila tulipopata mpira tulishambulia kwa haraka jambo ambalo lilitusaidia kuwapa presha wapinzani wetu na wakafanya makosa ambayo yakatupa ushindi.

“Mechi ilikuwa ngumu Ndanda ni timu nzuri lakini nashangaa hawapati matokeo mazuri katika mechi zao,” alisema Mkwasa.

Kocha msaidizi wa Ndanda Shaweji Nawanda alisema kosa walilofanya wachezaji wake limewagharimu, hivyo wanajipanga kwa mechi ijayo.

Wakati makocha wakitoa maoni hayo, mashabiki wa Yanga walisubiri hadi dakika ya 75 kushangilia bao la Sibomana aliyefunga kwa kiki ya mpira wa adhabu iliyomshinda kipa wa Ndanda Ally Mustapha ‘Barthez’ aliyewahi kucheza katika kikosi hicho.

Mpira wa adhabu ulitokana na makosa ya nahodha Aziz Sibo kushika mpira uliopigwa na Ngassa Yanga ilipofanya shambulizi la kushitukiza.

Awali mpira huo ulipigwa na David Molinga ambao uliwagonga baadhi ya wachezaji wa Ndanda, lakini mwamuzi Hans Mabena wa Tanga aliamuru adhabu hiyo irudiwe.

Uamuzi huo ulitokana na wachezaji wa Ndanda waliokuwa wameweka ukuta kuwahi kutoka eneo hilo kuzuia kabla ya Sibomana kupiga kiki hiyo.

Rekodi

Tangu mwaka 2014 Ndanda ilipopanda daraja imewahi kupoteza mara moja kwenye Uwanja huo dhidi ya Yanga.

Timu hizo zimekutana mara nne kwenye Uwanja wa Nangwanda Sijaona tangu mwaka 2014, huku kila timu ikishinda mara moja na zikitoka sare mara mbili.

Katika michezo hiyo Ndanda ilianza kuifunga Yanga bao 1-0 kwenye Uwanja huo Mei 9,2015 kisha zikatoka suluhu katika mechi iliyofanyika Septemba 7, 2016 kabla ya Yanga kushinda mabao 2-1 Februari 28, 2018 na msimu uliopita zilitoka sare ya bao 1-1.

Mchezo mmoja baina yao ambao ulikuwa ufanyike kwenye uwanja huo Mei 15,2016 ulihamishwa na kufanyika Taifa kwa makubaliano maalumu ya timu zote mbili. Mchezo huo ulimalizika kwa sare ya mabao 2-2.

Ndanda:Ally Mustafa, Aziz Sibo, Said Mbatty, Paul Mahona, Godfrey ,Malibich, Omari Hami Abdul Suleiman, Kassim Mdoe, Omary Issa na Hussein Javu.

Yanga: Farouk Shikalo, Juma Abdul, Jafari Mohammed, Kelvin Yondani, Ally Mtoni, Papy Tshishimbi, Deus Kaseke, Mapinduzi Balama, David Molinga, Raphael Daud na Parick Sibomana.

Advertisement