Simba, Nkana hesabu tupu

Thursday December 6 2018

 

By Khatimu Naheka, Mwananchi

Manzini. Ushindi mnono iliyopata Simba dhidi ya Mbabane Swallows ya Swaziland, umeacha maumivu nchini humo na sasa kigogo hicho kitakutana na Nkana Red Devils ya Zambia.

Nkana jana ilishinda bao 1-0 mjini Kitwe dhidi ya UD Songo ya Msumbiji. Katika mechi ya kwanza iliichapa mabao 2-1 mjini Maputo.

Mechi ya miamba hiyo itamrudisha nyumbani aliyekuwa beki wa Yanga, Hassani Kessy anayecheza soka ya kulipwa katika Klabu ya Nkana.

Simba imefuzu raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika, baada ya kusonga mbele kwa ushindi wa jumla wa mabao 8-1 iliyopata katika mechi mbili za nyumbani na ugenini.

Timu hiyo ilishinda mabao 4-1 katika mechi ya kwanza Dar es Salaam kabla ya juzi kuirarua Mbabane 4-0. Mabao ya Cletous Chama (mawili), Emmanuel Okwi na Meddie Kagere yalinogesha ushindi wa Simba.

Simba na Nkana zinakutana zikiwa ni klabu kongwe katika soka, Simba ikianzishwa mwaka 1936 wakati Nkana 1935 na jambo la kufurahisha timu zote mbili zinavaa jezi nyekundu.

Mechi hiyo itakuwa ya kulipa kisasi kwa Simba ambayo ilinyukwa na Nkana mwaka 2002 walipokutana kwa mara ya kwanza katika Ligi ya Mabingwa Afrika, hivyo ni hesebu pekee itakayotoa matokeo mazuri kwa timu itakayoshinda.

Katika mechi ya kwanza iliyopigwa mjini Kitwe, Nkana ilishinda mabao 4-0 na ziliporudiana Dar es Salaam, Simba ilishinda 3-0. Nkana ilisonga mbele kwa ushindi wa jumla wa mabao 4-3.

Lakini Simba ya sasa ni ya kuotea mbali kwa kuwa inajivunia ubora wa safu ya kiungo ikiongozwa na Mzambia Chama na ushambuliaji John Bocco, Emmanuel Okwi, Meddie Kagere.

Nayo Nkana inatambia nyota watatu tegemeo ambao ni mhimili wa matokeo mazuri inayopata akina Walter Bwalya, Kelvin Mubanga na Chisamba Lungu.

Tangu mwaka 1974, Simba imeshinda mara tatu kati ya mechi tano iliyocheza dhidi ya timu za Zambia katika mashindano ya Afrika.

Mwaka 1974, Simba ilitoa Green Buffaloes kwa jumla ya mabao 3-1 katika Kombe la Mabingwa Afrika. Awali, ilishinda 2-1 dhidi Buffaloes kabla ya kuilaza bao 1-0.

Mwaka 1976, Buffaloes iliing’oa Simba kwa jumla ya mabao 4-2, mechi ya kwanza Simba ilichapwa 3-2 na ziliporudiana ilifungwa bao 1-0.

Simba ilirudi Zambia mwaka 1995 na kufanikiwa kuitoa Power Dynamos kwa penalti 3-4 baada ya mechi mbili za nyumbani na ugenini kutoka sare ya bao 1-1, hivyo matokeo ya jumla kuwa 2-2 kabla ya kutumika kikwaju ya penalti.

Mwaka 2004, Simba ilitolewa katika Ligi ya Mabingwa Afrika na Zanaco baada ya kuchapwa jumla ya mabao 3-2. Mechi ya kwanza Simba ilishinda 1-0, lakini mechi ya marudiano Zanaco ilishinda 3-1 na kusonga mbele.

Ushindi wa kishindo iliyopata Simba unaweza kuwa kichocheo cha Simba kupata matokeo mazuri katika mchezo wake na Nkana hasa ubora wa kikosi cha Kocha, Patrick Aussems.

Hakuna aliyetarajia kama Simba ingepata ushindi huo kutokana na rekodi na ubora wa kikosi cha Mbabane katika mashindano ya kimataifa.

Uimara wa kikosi kipana unaweza kuwa chachu ya Simba kuanza vyema mchezo wa kwanza ambao utapigwa Desemba 14, 15 na 16 nchini Zambia kabla ya kurudiana Desemba 21 Dar es Salaam.

Akizungumza na gazeti hili jana kuhusiana na mechi dhidi ya Mbabane, Aussems alisema mbinu pekee aliyotumia kuizima Mbabane ni kucheza soka ya kufunguka licha ya kutangulia kupata ushindi mzuri nyumbani.

Aussems alisema Mbabane ilitarajia Simba itacheza mchezo wa kujilinda kwa kuwa ilikuwa na mtaji wa idadi kubwa ya mabao iliyopata katika mchezo wa kwanza.

“Nilijua nina timu imara yenye wachezaji wenye uwezo mzuri wa kucheza soka ya kufunguka. Pia nina vijana wanaojitambua wanaoweza kumiliki mpira, hivyo sikuwa na wasiwasi na mbinu niliyokuwa nimeandaa katika programu yangu,” alisema Aussems.

Kocha huyo alisema Mbabane ilipoteza mwelekeo katika mechi zote mbili kwa kuwa haikuwa na wachezaji wenye viwango bora wa kushindana na mastaa wake hasa katika eneo la kiungo.

“Tulidhibiti eneo la kiungo tukatengeneza nafasi. Unapokuwa na timu kama Simba kitu pekee unachotakiwa kukifanya ni kuwa mbunifu,” alisema Aussems.

Wakati huo huo timu ya JKU Zanzibar imefungwa mabao 2-0 na El Hilal ya Sudan, katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika uliochezwa jana kwenye Uwanja wa Amaan, Zanzibar.

Advertisement