Simba chama kubwa

Muktasari:

Kwa mujibu wa mazoezi hayo, staili ya kiuchezaji itabadilika na kuwapa nafasi kikosi cha kwanza baadhi ya nyota waliokuwa wakisotea benchi.

SIMBA kesho Alhamisi inaingia kwenye mtihani wa kwanza wa kuwakosa mastaa wao waliozoeleka kikosi cha kwanza tena ikicheza ugenini dhidi ya timu ngumu ya Prisons iliyotoka nayo suluhu nyumbani na ugenini msimu uliopita.

Hata hivyo, jana baada ya kutua Rukwa ilitamba itaonyesha kwa mara ya kwanza maana ya chama kubwa, huku Kocha Sven Vandebroeck akibadili mbinu mazoezini.

Watakaokosekana ni washambuliaji John Bocco na Meddie Kagere, pia kiungo mshambuliaji Clatous Chama na beki kisiki, Paschal Wawa wote kwa sababu tofauti.

Hata hivyo, benchi la ufundi la Simba limeamua kuja kivingine katika mchezo huo utakaopigwa Uwanja wa Nelson Mandela na kwa mujibu wa mazoezi ya juzi jioni na jana, huenda Prisons wakakumbana na sapraizi na sura mpya kadhaa kwenye kikosi cha kwanza.

Kwa mujibu wa mazoezi hayo, staili ya kiuchezaji itabadilika na kuwapa nafasi kikosi cha kwanza baadhi ya nyota waliokuwa wakisotea benchi.

Winga Bernard Morrison, mshambuliaji Ibrahim Ajibu na beki Kennedy Wilson huenda wakaanza. Lakini tofauti na ilivyozoeleka kwa Morrison kucheza nafasi ya kiungo wa pembeni au winga, safari hii huenda akapangwa kama mshambuliaji wa kati sambamba na Chris Mugalu.

Utulivu wa Morrison, chenga, kasi na uwezo wa kupiga pasi ya mwisho ama kufunga kunaweza kuilazimisha Simba kumlisha idadi kubwa ya mipira jambo litakalompa fursa Mugalu kujipanga na kusimama katika eneo sahihi katika lango la adui pindi wanaposhambulia.

Morrison aliifanyia majaribio nafasi hiyo katika mechi ya kirafiki dhidi ya Mlandege na hivyo kutailazimisha Simba ishambulie zaidi kupitia katikati badala ya kutegemea pembeni kupitia mipira ya krosi kama ilivyofanya dhidi ya JKT Tanzania.

Nyuma yao wanaweza kupangwa viungo watatu wa ushambuliaji ambao watakuwa ni Ibrahim Ajibu na Luis Miquissone ambao watakuwa wakicheza pembeni ya Larry Bwalya wakiwa na jukumu la kuwalisha mipira washambuliaji wa kati.

Hata hivyo, mara kwa mara Ajibu amekuwa akifanya vizuri zaidi pindi anapopangwa kucheza nafasi ya nyuma ya mshambuliaji wa kati ambayo dhidi ya Prisons atapangwa Bwalya.

Ajibu tangu msimu huu ulipoanza, hajafanikiwa kuwemo kikosi cha kwanza katika mechi zote za mashindano walizocheza huku pia katika safu ya ulinzi, beki Kennedy Wilson baada ya kusotea benchi tangu alivyocheza dhidi ya Mtibwa Sugar, huenda akarudi kikosini kutokana na kukosekana kwa Serge Wawa.

Hata hivyo, wachezaji wengine ambao kocha Sven anaweza kuwatumia kuziba nafasi za wanaokosekana ni Francis Kahata, Miraji Athuman na Hassan Dilunga katika eneo la ushambuliaji au kiungo lakini katika ukuta, anaweza pia kumtumia beki Erasto Nyoni.

Kocha Sven alikiri kikosi chake kitakuwa na mabadiliko kadha kutokana na kuwakosa baadhi ya wachezaji.

“Baadhi ya wachezaji tutawakosa kwa kuwa hawatosafiri lakini waliobakia wanaweza kutimiza vyema majukumu yao ndani ya uwanja ingawa tunatakiwa turekebishe baadhi ya kasoro kama vile kutengeneza nafasi.

Mechi dhidi ya Mlandege imetusaidia kwa sababu wapinzani walikuwa wanacheza kwa kutumia nguvu jambo ambalo tulihitaji kukutana nalo ili tuweze kuona tunalikabili vipi,” alisema Sven.