Simba kicheko, Azam majanga

Sunday February 16 2020

 

By Godfrey Kahango, Mwananchi

Iringa. Wakati Simba ikiendeleza ubabe katika Ligi Kuu Tanzania Bara, Azam imegeuka mteja wa Coastal Union baada ya jana kufungwa mara ya pili.

Bao la nahodha John Bocco alilofunga dhidi ya Lipuli kwenye Uwanja wa Samora, Iringa limezidi kuipaisha Simba katika msimamo wa Ligi Kuu. Simba ilishinda bao 1-0.

Mshambuliaji huyo alifunga bao hilo dakika ya 23 kwa kiki ya mguu wa kushoto iliyompita kipa Deo Munishi ‘Dida’ baada ya kupata pasi ya Francis Kahata.

Matokeo hayo yameifanya Simba kujikita kileleni kwa pointi 56. Kabla ya mchezo wa jana, timu hiyo iliilaza Mtibwa Sugar mabao 3-0.

Kocha wa Simba, Sven Vandensbroek alisema licha ya kupata ushindi, wachezaji wake walikosa nafasi nyingi za kufunga.

“Tumepoteza nafasi nyingi kutokana na viatu vya wachezaji kutomudu hali ya uwanja sababu ya tope, lakini nawapongeza walipambana na tumepata ushindi,” alisema kocha huyo.

Advertisement

Kocha wa Lipuli Julio Elieza alisema hawezi kuwalaumu wachezaji kwa matokeo hayo kwa kuwa ni sehemu ya mchezo.

“Siwezi kuwalaumu wachezaji wamecheza mpira vizuri na wamejitahidi kadiri ya uwezo wao lakini bahati haikuwa kwetu. Simba wamepata nafasi nyingi lakini moja imewapa ushindi,”alisema Elieza.

Wakati Simba ikivuna pointi tatu, Azam ilionja shubiri ilipofungwa bao mabao 2-1 na Coastal Union kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.

Mabao ya Coastal yalifungwa na Ayoub Lyanga dakika ya 36 na Mudathir Said dakika 64. Azam ilipata bao dakika ya Obrey Chirwa dakika ya 93.

Azam imepoteza kwa mara ya pili mchezo wake wa Ligi Kuu baada ya mechi ya mzunguko wa kwanza iliyochezwa Uwanja wa Mkwakwani, Tanga kuchapwa bao 1-0.

Kocha msaidizi wa Azam Idd Nassor ‘Cheche’ alisema wachezaji wake walishindwa kufuata maelekezo ya benchi la ufundi wakati wakijiandaa na mchezo huo.

“Wachezaji wangu hawakufuata maelekezo tulipofungwa bao la kwanza liliwaondoa mchezoni, napongeza bao la mfungaji wa Coastal ni kijana anayekuja vizuri,”alisema Cheche.

Aidha, jahazi la Singida United limeendelea kuzama baada ya kufungwa bao 1-0 dhidi ya Ndanda. Matokeo hayo yamezidi kuiweka pabaya timu hiyo katika shimo la kuteremka daraja.

Wakati Ndanda ikiendelea kusogea juu ya msimamo kwa kufikisha pointi 22, Singida inaendelea kuburuza mkia ikiwa na pointi 11. Timu hiyo imefungwa mechi 15 kati ya 22 ilizocheza msimu huu.

Lipuli: Deo Munishi, David Kameta, Paul Ngalema, Peter Mwangosi, Novatus Lufunga, David Majinge, Mwinyi Ahmad, Fred Tangalo, Joshua Ibrahim, Daruweshi Saliboko na Keneth Masumbuko.

Simba: Aishi Manula, Shomari Kapombe, Mohammed Hussein, Kennedy Juma, Pascal Wawa, Jonas Mkude, Hassan Dilunga, Clatous Chama, Meddie Kagere, John Bocco na Francis Kahata.

Matokeo ya mechi nyingine, Polisi Tanzania iliichapa KMC mabao 3-2, Namungo ilitoka sare ya bao 1-1 dhidi ya Mwadui, Ruvu Shooting ilishinda 1-0 ilipovaana na Mbeya City ambayo ipo katika janga la kujinasua kushuka daraja.

Biashara United ikiwa nyumbani kwenye Uwanja wa Karume mkoani Mara iliilaza Alliance bao 1-0, Kagera Sugar iliinyuka Mbao mabao 2-0, Singida United ilinyukwa 1-0 dhidi ya Ndanda.

Advertisement