Simba yaanza na wapya watano

KAMA mikakati ya Simba ikienda sawa huenda wakamaliza usajili kabla ya msimu huu wa Ligi Kuu Bara haujamalizika na kuweka historia ya aina yake.

Mwanaspoti limethibitishiwa na Ofisa Mtendaji Mkuu wa Simba, Senzo Mazingisa kwamba wamepokea ripoti ya awali kutoka kwa kocha, Sven Vendenbroeck inayohitaji mastaa watano wa maana.

Senzo amebainisha kwamba jambo la kwanza Kocha anataka wachezaji wasizidi watano tu na wao kama uongozi wamempa nafasi ya kutaja wachezaji ambao anawataka ili kuona kama wana uwezo kuwasajili. Senzo anasema amewaambia anataka mastraika wawili, kiungo mwenye uwezo wa kucheza kwenye kukaba na kushambulia pamoja na beki wa kati lakini na Wabongo kadhaa.

Anasema wao uongozi wamempa nafasi hiyo mapema Sven kutaja wachezaji ambao anawataka ili kupunguza presha ya usajili pindi dirisha litakapofunguliwa na si kama kila mchezaji ambaye atakuwa amependekeza atasajiliwa kwani katika kila eneo moja ambalo anataka kutakuwa na wachezaji watatu chaguo la kwanza.

“Katika hili la usajili tumeanza tayari skauti katika maeneo mengi hapa Afrika ili kupata wachezaji bora na imara pengine tutafanya usajili mzuri kuliko misimu yote kwani kuna vigezo vingi kulingana na mahitaji yetu. Hatutasajili kwa mihemko,” alisema.

“Jambo la pili, Sven amependekeza kutoa ruhusa kwa wachezaji wale ambao hawakuwa wanapata nafasi ya kucheza mara kwa mara kwenda katika timu nyingine hata kama wakiwa bado wana mikataba au wamemaliza

“Suala la tatu ambalo Sven aliweka katika ripoti yake ni kwamba skauti ifanyike kwa kutumia kampuni ambazo zinaweza kumuangalia mchezaji na kumuelezea ubora na udhaifu wake, zoezi hilo lilifanyika kwenye usajili wa msimu uliopita tukitumia moja ya kampuni za Afrika Kusini.

“Jambo la nne, Sven amewataka wachezaji wake huko walipo wajilinde na Corona pamoja na kufanya mazoezi peke yao, lakini kuweka miili yao sawa ili kumalizia vizuri mechi zilizobaki na kukamilisha malengo yao ya kutwaa ubingwa wa ligi msimu huu,” alisema Senzo.

“Suala la mwisho tumeanza kuangalia wachezaji katika ligi ya ndani ambapo tunaweza kusajili hata wawili na maeneo mengine Afrika katika nchi ambazo zimeendelea kisoka,” alisisitiza Senzo.

Mwanaspoti linajua kwamba wachezaji waliopo kwenye rada ya Simba kwa sasa ni Msierra Leone, Sheka Fofanah anayekipiga Arabuni, Mpiana Mozizi wa FC Lupopo ya DR Congo.

Mastaa wa ndani ambao pia wamo kwenye uteuzi wa Taifa Stars ni Reliants Lusajo na Lucas Kikoti wote wa Namungo pamoja na beki wa kati wa Coastal Union Bakari Nondo ‘Mwamnyeto’.

Simba imedhamiria kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Bara kwa msimu wa tatu mfululizo huku pia ikilitaka Kombe la Shirikisho ambalo liko hatua ya robo fainali.