Singano aoga mamilioni TP Mazembe

Dar es Salaam. Nyota wa zamani wa Azam FC, Ramadhani Singano ‘Messi’ aliyesajiliwa na TP Mazembe ya Lubumbashi nchini DR Congo anakwenda kuvuta fedha za maana, baada ya kukamilisha usajili wake wiki hii.

Singano ametia saini mkataba wa miaka minne ulioigharimu Sh125 milioni timu hiyo ambayo imewahi kuchukua ubingwa wa Afrika mara tano.

Sambamba na mkataba huo, pia kila mwezi atakuwa analipwa Dola 4,000 za Marekani (zaidi ya Sh9 milioni). Wakala wa mchezaji huyo, Rashid Ally amesema Singano amesaini mkataba wa miaka minne baada ya mmiliki wa timu hiyo, Moise Katumbi kuziona video zake ambapo alisisitiza nyota huyo atue kikosini.

Sambamba na Messi, pia katika safari yake ilikuwa aende na Mrisho Ngassa, lakini ameshindwa kwenda baada ya Yanga kumuwekea mezani fedha, akasaini.

“Safari (yake Messi) ilikuwa aende kwanza Katanga, lakini Don Bosco wakampenda. Baadaye kocha wa Don Bosco akamwonyesha Katumbi zile video ndio akamwambia huyu ni wa kucheza TP Mazembe. Ilikuwa aende na Ngassa lakini ndio hivyo, mambo hayakwenda sawa,” alisema Ally.

Alisema TP Mazembe ni klabu kubwa Afrika na upo uwezekano Singano akawa na maisha mazuri zaidi katika timu hiyo endapo ataonyesha kiwango cha juu. Singano alisaini mkataba huo wiki hii katika ofisi za Katumbi zilizopo jijini Lubumbashi baada ya kuachwa huru na Azam FC.

Nyota huyo aliyewahi pia kuichezea Simba atakuwa sehemu ya wachezaji wa kikosi hicho kuanzia msimu ujao na atakuwa pamoja na Mtanzania mwingine Eliud Ambokile.

Singano aliondoka nchini Jumanne wiki hii kwa ndege ya Shirika la Kenya akipitia Nairobi.

Awali, kabla ya kusajiliwa kwake TP Mazembe ilikuwa ikimfukuzia Ibrahim Ajibu ambaye alikataa na kujiunga na Simba akitokea Yanga. Singano anakuwa mchezaji wa pili Mtanzania kusajiliwa na TP Mazembe msimu huu baada ya Ambokile.

Kabla ya nyota hao kujiunga na timu hiyo, miaka iliyopita wachezaji Mbwana Samatta anayekipiga Genk ya Ubelgiji, Thomas Ulimwengu wa JS Saoura ya Algeria na Ngawina Ngawina waliwahi kuichezea.