Singida, Mbeya City zapumulia mashine Ligi Kuu Tanzania Bara

Dar es Salaam. Wakati Ligi Kuu Tanzania Bara ikiingia raundi ya 22, vita ya kuwania kubaki katika mashindano hayo ni jambo jingine ambalo limeonekana kukoleza ushindani msimu huu.

Tofauti na misimu ya nyuma ambapo timu chache zilikuwa zikishuka daraja hali ni tofauti msimu huu ambapo huenda ukaweka historia.

Kwa mujibu wa kanuni za Ligi Kuu, upo uwezekano wa timu sita kushuka daraja msimu ujao ili kutoa fursa ya kupunguza idadi ya timu katika ligi.

“Timu 4 (nne) za mwisho, zilizoshika nafasi ya 17 hadi 20 kwenye Ligi Kuu zitashuka moja kwa moja kucheza Ligi Daraja la Kwanza (FDL) msimu unaofuata,” inafafanua ibara ya tatu (3) ya kanuni ya tano (5) ya ligi hiyo msimu huu.

Kanuni hiyo pia inafafanua timu mbili ile iliyoshika nafasi ya 15 na 16 katika msimamo wa ligi pindi msimu utakapomalizika zitacheza mechi za mchujo (play off) dhidi ya timu mbili za Ligi Daraja la Kwanza (FDL) na ikiwa zitapoteza zitashuka daraja.

Kuna kundi la timu tisa, lakini nne zitashuka daraja na mbili kati ya hizo zitaangukia katika mchujo ingawa pia zinaweza kuchanga karata vyema na kubaki ni Singida United, Mbeya City, Mwadui, Mbao, Ndanda, KMC, Alliance, Ruvu Shooting na Mtibwa Sugar.

Singida United

Tofauti kubwa ya pointi baina yake na timu za juu yake unaiweka katika mazingira magumu Singida United kubaki Ligi Kuu.

Ikiwa imecheza michezo 21, ina pointi 11 ambazo ni saba pungufu ya zile za timu iliyo nafasi ya 19, Mbeya City ambayo ina pointi 18.

Katika michezo 17 iliyobakiza, itacheza michezo tisa nyumbani na nane ugenini. Katika michezo tisa ya nyumbani, ambayo ina uhakika angalau wa kuibuka na ushindi ni minne.

Mbeya City

Imeonekana kuimarika katika siku za hivi karibuni baada ya kufanya usajili wa dirisha dogo na kuimarisha benchi la ufundi kwa kumleta kocha Amri Said.

Ina pointi 18 na imebakiza michezo 17 ambapo nyumbani minane. Kwa uimara wao wa sasa wana uwezo wa kupata ushindi wa takribani mechi saba kati ya hizo na kwa zile wanazoweza kutoka sare wanaweza kucheza mchujo lakini wasipokuwa makini watashuka.

Mwadui

Msimu uliopita ililazimika kucheza mchujo ndipo ikafanikiwa kubaki Ligi Kuu lakini kwa hali ilivyo msimu huu huenda ikajikuta shimoni.

Matokeo ya sare yamekuwa yakiwaangusha na siku za karibuni imekuwa haina muendelezo mzuri wa ubora jambo ambalo limewagharimu.

Mbao

Haina rekodi nzuri uwanja wa nyumbani ambapo katika michezo 11, imeshinda mara mbili, sare nne na kupoteza mitano huku ugenini ikipata ushindi mara mbili, sare tatu na kupoteza mitano.

Imebakiza idadi ya michezo sita. Ugenini mechi 13 nyingi dhidi ya timu zilizovuna pointi katika uwanja wake wa nyumbani.

KMC

Ina faida ya kuwa na idadi kubwa ya mechi za nyumbani mzunguko wa pili ambapo itacheza 10 jambo ambalo linawaweka katika nafasi nzuri ya kubaki ingawa inapaswa kujipanga kikamilifu.

Alliance

Changamoto kubwa inayoikabili Alliance ni kama ile ya Mbao ambayo ni kushindwa kutumia vyema uwanja wa nyumbani licha ya kujitahidi inapokuwa ugenini.

Ruvu Shooting

Imekuwa ikinufaika na uwanja wa nyumbani lakini haina rekodi nzuri ugenini. Kwa nafasi waliyopo wanaweza kubaki lakini wakiendeleza kupoteza pointi ugenini watajikuta pabaya.

Ndanda

Imekuwa ikitumia vyema uwanja wa nyumbani ingawa ina changamoto ya kutofanya vizuri ugenini. Haina idadi kubwa ya mechi ngumu nyumbani ambako katika mechi 10, imeshinda mara tatu, sare tatu na kupoteza tatu.

Kocha wa Mbeya City, Amri Said alisema wana nafasi ya kubaki Ligi Kuu kwa kuwa kikosi chake kimeimarika baada ya kufanya usajili katika dirisha dogo.

Kocha wa Ndanda Abdul Mingange alisema watazitumia vyema mechi zilizobaki ili kubaki katika mashindano hayo ingawa haitakuwa kazi nyepesi kutokana na ushindani uliopo.