Siri ya ushindi Yanga hii hapa

Muktasari:

Ushindi huo unawafanya vijana hao wa Jangwani kufikisha alama 61 na kuendelea kujiimarisha kileleni kwenye msimamo wa Ligi Kuu.

Mwanza. Nidhamu ya washambuliaji wa Yanga jana ilikuwa silaha ya kuvunja mwiko wa Mbao FC na kuondoka na pointi tatu ugenini.

Yanga iliondoa unyonge kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, baada ya kuichapa Mbao mabao 2-1 katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Kocha Mwinyi Zahera ametoboa siri ya ushindi huo. Kocha huyo alisema baada ya kusoma mchezo, alibaini Mbao haina mabeki imara wa pembeni, hivyo alitoa maelekezo kwa viungo wa pembeni kutumia fursa hiyo.

“Baada ya kwenda mapumziko, niliwaambia watumie zaidi mipira ya pembeni, kupiga krosi nyingi badala ya kupita katikati,” alisema Zahera.

Mchezo wa jana ulikuwa wa nne kwa timu hizo. Msimu 2016/2017 Yanga ilifungwa bao 1-0 katika Ligi Kuu na Kombe la FA. 2017/2018 Yanga ilifungwa mabao 2-0 katika Ligi Kuu.

Mabao mawili yaliyofungwa na Heritier Makambo na Amissi Tambwe yaliongeza pengo la pointi baina yao na Azam. Yanga imefikisha pointi 61 Azam (50) na Simba (42). Zahera alimuanzisha Abdallah Shaibu badala ya Andrew Vincent. Pia alimtumia Haruna Moshi ‘Boban’, Papy Tshishimbi kuanza katika kiungo.

Makambo na Tambwe waliocheza pacha walikuwa mwiba kwa mabeki wa Mbao kutokana na kufanya mashambulizi ya mara kwa mara langoni. Katika kudhihirisha makali yao Makambo, alikosa bao dakika ya sita alipotengewa pasi na Mrisho Ngassa.

Pia Tambwe alikosa bao dakika 23 alipounganisha vibaya mpira wa krosi uliopigwa na Paul Godfrey ‘Boxer’. Makambo alifunga bao lake la 12 msimu huu dakika ya 50 kwa mpira wa kichwa akiunganisha krosi ya Tshishimbi iliyotoka upande wa kulia. Mbao ilitangulia kufunga dakika ya 45 baada ya Ndaki Robert kuunganisha krosi iliyopigwa na Amos Charles. Bao hilo lilitokana na uzembe wa kipa Ramadhani Kabwili aliyeshindwa kucheza mpira huo wa krosi uliopigwa kutoka upande wa kushoto.

Dakika ya 68 Yanga ilipata bao la pili lililofungwa kwa penalti na Tambwe baada ya beki wa Mbao Balilas Chitembe kushika mpira ndani ya eneo la hatari.

Katika mechi nyingine, Ndanda iliichapa Singida United 2-0, Prisons iliilaza Mbeya City 1-0, Lipuli ilichapwa 3-2 na Stand, KMC ilishinda 1-0 dhidi ya Mtibwa.

Mbao: Metacha Mnata, Vincent Philip, Amos Charles, David Mwassa, Erick Mulilo, Ally Mussa, Said Said, Ibrahim Hashimu, Pastory Athanas, Benard Gernas na Ndaki Robert.

Yanga: Ramadhani Kabwili, Paul Godfrey, Haji Mwinyi, Kelvin Yondani, Abdallah Shaibu, Papy Tshishimbi, Mrisho Ngassa/Mohammed Issa, Haruna Moshi, Heritier Makambo, Amissi Tambwe/Andrew Vincent na Ibrahim Ajibu.