Solskjaer aanza kuchapwa Man United

London, England. Uamuzi wa kocha wa Manchester United, Ole Gunnar Solskjaer, wa kugawa sawa majukumu ya kupiga penalti kikosini mwake, umetajwa kuwa ni ’mambo ya kitoto’ na nyota wa zamani wa timu ya taifa ya England, Matt Le Tissier.

Mashetani Wekundu walikosa ‘matuta’ mfululizo katika mechi dhidi ya Wolves na Crystal Palace mapema msimu huu baada ya Paul Pogba na Marcus Rashford wote kushindwa kufunga penalti zao.

Kutokana na kukosa huko, Solskjaer alilazimika kufafanua kuwa wawili hao wanaamua wenyewe nani apige penalti msimu huu – hali ambayo Le Tissier anaona ni udhaifu mkubwa wa kiuongozi.

“Lazima italeta mvurugano kama unakuwa na wapiga penalti wawili kisha unakaa kando kuwaangalia ukijisemea, ‘Hebu tuone nani atatamani zaidi kupiga penalti leo’,” Le Tissier alisema.

“Huo sio weledi, ni utoto, mambo ya kishule shule hayo na lawama zinarudi kwa kocha. Katika hali kama ile, kocha anapaswa kuwa ngangari na kuamua, ‘Wewe ndiye bora katika upigaji wa penalti, utakuwa mpiga penalti wangu, kama hautakuwapo uwanjani yeye atapiga, lakini hadi hilo litokee, vinginevyo utapiga wewe’.

“Tulikuwa na mashindano ya kupiga penalti mazoezini ya kuamua nani atakuwa mpigaji wa kudumu wa penalti wakati wa mechi na nilishinda mimi. Nilikuwa na umri wa miaka 20 niliposhinda nafasi ya kuwa mpigaji wa penalti wa timu na kuanzia hapo hapakuwa na maswali tena nilipokuwapo uwanjani, ilikuwa ni haki yangu na ilikuwa ni kazi yangu.”

Le Tissier, ambaye alicheza zaidi ya mechi 400 akiwa na Southampton, alikosa penalti moja tu kati ya 48 alizopiga katika maisha yake ya soka, huku kipa wa

Nottingham Forest, Mark Crossley akiwa mtu pekee aliyeokoa penalti yake mwaka 1993.

Gwiji huyo anasema kama angekuwa anaamua yeye, angemchagua Rashford, 21, kuwa mpigaji wake wa kudumu wa penalti kwa sababu anakuwa ‘siriasi’ anapoelekea kupiga penalti tofauti na Pogba ambaye anapiga hatua kuelekea kupiga ‘tuta’ utadhani anaigiza filamu ya Hollywood.