Stars ni mbele kwa mbele

Monday November 18 2019

 

By Thomas Ng’itu, Mwananchi tng’[email protected]

Kuanzia nyumbani kuna raha yake, asukuambie mtu. Kuanzia nyumbani kwa timu ya Taifa ‘Taif Stars’ katika mchezo wa kufuzu Afcon dhidi ya Guinea kulitoa taswira mapema ya kuibuka na ushindi katika mchezo huo ambao ulimalizika kwa ushindi wa mabao 2-1.

Hali hiyo pengine ilichagizwa na kupata matokeo mazuri katika uwanja huo katika miaka ya karibuni, huku ule wa kukumbukwa ukiwa ni pale walipoifunga Uganda na kufuzu michuano ya Afcon iliyofanyika mwaka huu kule Misri.

Guinea waliingia uwanjani

huku wakidhamiria kutaka kumaliza mechi mapema katika dakika za mwanzo, na walifanikiwa kupata bao katika dakika ya 15.

Hata hivyo, wingi wa mashabiki waliojitokeza katika uwanja huo ulizidisha ari ya Stars kufanya kweli, na uliwafanya Guinea kukubali kwamba wapo ugenini.

Mashabiki wa Tanzania katika kipindi cha pili waliondoa uchovu walioupata kipindi cha kwanza baada ya kufungwa bao la mapema na kuanza kushangilia kwa dakika zote zilizosalia.

Advertisement

Hali hiyo ilirejesha morali kwa wachezaji na kusawazisha bao katika dakika ya 68 lililofungwa na Saimon Msuva kabla ya Salum Aboubakar ‘Sure Boy’ kulihakikisha taifa ushindi. Yote kwa yote imani ambayo Kocha Etienne Ndayiragije aliipata kutoka kwa mashabiki wa Tanzania inaweza kuwa ilichangia kumfanya ‘ajilipue’ katika kipindi cha pili kwa kufanya mabadiliko.

Ndayiragije alionyesha umahiri wake katika kipindi hicho baada ya kuachana na mfumo wa 4-4-2 na kutumia ule wa 3-4-3 uliolenga kuwa na washambuliaji watatu badala ya wawili.

Etienne alifumba macho na kumtoa Hassan Kessy upande wa kulia na kumuingiza Ditram Nchimbi kwenye eneo la ushambuliaji. Mabadiliko hayo aliyafanya zaidi akilenga matokeo ambayo kipindi cha kwanza yalionekana kuwa magumu, kwani Guinea walimkomalia mwanzo mwisho mshambuliaji wa kimataifa wa Tanzania, Mbwana Samatta.

Baada ya kuingia kwa Nchimbi ndipo Ndayiragije akabadili mfumo na kucheza 3-4-3 uliozalisha mabao hayo, ikizingatiwa kwamba kuingia kwa mshambuliaji huyo kuliwafanya Guinea sasa kuhaha kuwazuia washambuliaji watatu Samatta, Msuva na Nchimbi.

Advertisement