Straika mpya wa Yanga aja na neema

Dar es Salaam. Usajili wa mshambuliaji mpya wa Yanga, Tariq Seif Kiakala umefuatana na neema baada ya wadhamini kampuni ya GSM kutangaza zawadi ya Sh. 10 milioni kwa wachezaji kila timu inapopata ushindi.

Tariq alikamilisha usajili wake Yanga jana baada ya kumwaga wino wa kuitumikia klabu hiyo ya Jangwani kwa misimu miwili.

Usajili huo wa mapema umefanyika kabla ya dirisha la uhamisho kufunguliwa kesho ili baadaye aidhinishwe kuitumikia klabu hiyo.

Kutua kwa Tariq anayejua kufunga mabao magumu akifanya hivyo kwa kuzitungua timu mbalimbali zikiwamo Simba na Yanga msimu uliopita, alipokuwa na Biashara United kabla ya kutimkia Misri ambako uhamisho wake ulikwama, anaingia kwenye timu hiyo kushusha presha ya mashabiki wao baada ya kuondoka na washambuliaji wawili wa kigeni Sadney Urikhob na Juma Balinya.

Wawili hao waliachana na Yanga wiki hii baada ya kuomba kuvunja mikataba kwa kuchelewa kulipwa mishahara yao na klabu hiyo kuridhia wakidai nao walikuwa wanawapigia hesabu za kuwatema.

Mwenyekiti wa Yanga Dk Mshindo Msolla ametumia nafasi hiyo kuwashusha presha mashabiki wa timu hiyo akisema licha ya changamoto mbalimbali za kiuchumi wanaendelea kupambana kuisuka timu hiyo na kwamba Tariq ametangulia tu.

“Tuna furaha kukamilisha usajili huu muhimu wa Kiakala ambaye kazi yake inajulikana kwa wanaofuatilia mpira hapa nchini wanajua Yanga tumechukua mchezaji wa namna gani,” alisema Msolla.