TCU yavionya vyuo vinavyosuasua kuwahamisha wanafunzi

Friday November 9 2018

 

By Kalunde Jamal, Mwananchi

Dar es Salaam. Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) imetoa maelekezo kwa vyuo vyote vinavyotakiwa kuhamisha wanafunzi kuzingatia taratibu ikiwamo kutoa mwongozo wa namna ya kuhama.

Maelekezo hayo yamekuja baada ya kuwapo kwa mkanganyiko hapo kabla inapotokea vyuo kutakiwa kuwahamisha wanafunzi kwa sababu mbalimbali ikiwamo kufutiwa usajili.

Akizungumza na waandishi wa habari leo, Ijumaa Novemba 9, 2018, Katibu Mtendaji wa TCU, Profesa Charles Kihampa amesema vyuo vikuu vyote vinavyotakiwa kuwahamisha wanafunzi kufuata taratibu za uhamisho ikiwamo kukamilisha shughuli ya uhamisho ndani ya wiki mbili kuanzia Novemba 7, 2018.

Profesa Kihampa ameviagiza vyuo vikuu ambavyo wanafunzi wao wanatakiwa kuhama kuwasiliana haraka na vyuo wanavyotakiwa kuhamia na kuwasilisha taarifa zote zinazowahusu kwa vyuo wanavyohamia.

 

"Tume inaviagiza vyuo vikuu vyote vilivyoelekezwa kuhamisha wanafunzi kuwaarifu mara moja wanafunzi wote kuhusu vyuo wanavyotakiwa kuhama kama walivyoelekezwa," amesema Profesa Kihampa.

 

Hivi karibuni Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom) kilikataa kuwapokea wanafunzi 138 wa Chuo Kikuu Kishiriki cha Josiah Kibira (JoKUCo) waliokwenda hapo kwa lengo la kuhamia katika chuo hicho kilichopo jijini Dodoma, kwa maelezo kwamba hakiwatambui.


Chuo cha Josiah Kibira cha Chuo Kikuu cha Tumaini Makumira (Tuma) kilifikia uamuzi wa kuwahamishia Udom wanafunzi hao kutekeleza agizo la TCU la Septemba 25, baada ya kusitisha utoaji wa mafunzo kwa ngazi zote kwenye vyuo vitano kikiwamo cha Josiah Kibira.

 

Advertisement