Taifa Stars na jasho la thamani

Ilipita miaka 39 tangu mara ya mwisho tushiriki mashindano ya Mataifa ya Afrika.Ni kipindi kirefu ambacho mengi yalikuwa hayapo hivi yalivyokuwa leo, kipindi kirefu ambacho hakuna picha za kumbukumbu ya kilichotokea na ndio maana hatufahamu namna mastaa wa kipindi hicho walivyofanya balaa. Hatuna picha kwenye medula zetu kwa sababu teknolojia haikuturuhusu na hata kama zilikuwepo picha za “black and white” waliokuwepo kipindi hicho hawakuona umuhimu mkubwa wa kufanya hivyo.

Hata historia ukiitafuta kuanzia shirikisho la soka Tanzania bara (TFF), mpaka wizarani kuna vitu huwezi kuvipata. Maana yake ni kuwa Taifa halikuwa na kumbukumbu kamili za kimaandishi na picha zaidi ya simulizi ambazo zilibaki kuwa simulizi kama za babu zetu kwa wale ambao wana umri huo na kushuka chini. Mwaka 2019, unazalisha wanahistoria wengine, unazalisha Leodger Chilla Tenga mpya, Peter Tino na Athumani Mambosasa na akina Jella Mtagwa wapya.

Unapokuwa kwenye kochi unatazama Samatta na kitambaa cha unahodha unatazama historia, Aishi Manula golini ni historia na Kelvin Yondani anapopambana na Mohamed Salah ni historia pia. Lakini kuna ule wakati ambao tukiwa na glasi mezani za vinywaji tofauti tutasimama tukiwa huku Tanzania, na tutaimba kwa pamoja majumbani mpaka kwenye vibanda umiza wimbo wa Taifa pamoja na wachezaji wetu wanaotetea Taifa wakiwa nchini Misri. Heshima ya kipekee kuwepo wakati huu na ni historia ya kipekee kushuhudia tukio hili.

Tunatakiwa kushikilia hii kumbukumbu kwa sababu inaweza kuishi kwa kipindi kirefu na tukawa hatuna haja ya kuwasimulia wanetu na wajukuu mengi kwa sababu kumbukumbu za picha zitafanya kazi kubwa.

Wakati ikiwa historia kwa Taifa na sisi wananchi yake, hii ni historia tofauti kidogo kwa wachezaji wetu, huu ni wakati tofauti kwa Ally Sonso wa Lipuli ni fursa ya kipekee kwa Hassani Kessy, Feisal Salum, Vincet Philipo na akina Gadiel Michael. Huu ni wakati wa kubadili fikra, wakati wa kuona maghorofa pamoja na kwamba wameshakua, wakati wa kutoa ushamba na wakati wa kufanya maisha yao kuwa tofauti. Wamecheza mechi ya kirafiki dhidi ya Mo Salah, Mohamed Elneny, Ahmed Hegazi na Ali Ghazal wa Misri ambao walishuhudia mara nyingi wakicheza zao kule Ulaya hususani Ligi Kuu nchini England. Kisha watacheza na Sadio Mane bingwa wa Klabu bingwa barani Ulaya, watakutana pia na Riyad Mahrez bingwa wa ligi kuu nchini England. Hizi ni mechi ambazo sio tu sisi Watanzania tutakuwa tunazitazama bali maskauti wa timu mbalimbali barani Ulaya na Afrika kwa ujumla watakuwa wanazitolea macho makali zaidi yetu. Wao hawatakuwa na shauku bali umakini wa mchezaji gani anawafaa kwenye dirisha hili la usajili.

Huu ndio wakati pekee wa wachezaji wetu kutizama akaunti zao za benki na kisha kufananisha na zile za wanaoenda kukabiliana nao kisha wapige goti na kusali na kuhakikisha kuwa jasho linalomwagika uwanjani ni jasho la thamani, jasho lenye kushika macho ya maskauti na jasho ambalo litatufanya watanzania tujipige vifuani kwa faraja.

Huu ni wakati ambao mataifa 24 pekee yatakuwa yanatazamwa duniani kote kutokea Afrika. Muda pekee ambao wachezaji 552 kati ya wachezaji maelfu kutokea Afrika watakuwa wanatizamwa kutokea kila pembe ya dunia kutokea kila ligi na klabu tofauti na wachezaji wetu ni sehemu ya idadi hiyo ya wachezaji. Wakiwa wanaitizama mitaa ya Misri, viwanja vyake na Piramids za kihistoria wanatakiwa wakumbuke pia pale ndipo sadaka yao ilipo. Pale ndipo ambapo baraka zimelal. Kila historia itaandikwa hapo na inaweza kutuchukua muda kurejea na ni wakati wao kufurahia historia hii. Kuna namna moja tu ya kufanya hivi kuvuja jasho la thamani. Jasho la thamani ndio muhimu.