‘Tutapigana dakika zote 90’

Dar es Salaam. Wakati Simba ikiikabili TP Mazembe kwenye mchezo wa pili wa hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, kocha wake, Patrick Aussems amesema watapambana dakika zote 90. Mchezo huo umepangwa kufanyika Stade TP Mazembe, Lubumbashi DR Congo.

Awali kwenye mchezo wa kwanza wa robo fainali uliopigwa Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam wiki moja iliyopita, Simba ambao ni wawakilishi wa Tanzania kwenye mashindano hayo walibanwa mbavu na kwenda suluhu.

Kikosi kamili cha Simba kikiongozwa na nahodha wao, John Bocco kiliondoka jana asubuhi kwa ndege ya kukodi kikiwa na wachezaji 18 tayari kwa mchezo huo wa marudiano.

Kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa Kimataifa wa Julius Nyerere (Terminal 1) Aussems alisema wamejiandaa kwa wiki moja kwenda kutafuta matokeo ya ushindi Lumbambashi ili kutinga nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Katika wiki hiyo Simba walianza maandalizi yao kwa kujikita na mazoezi ya kujenga utimamu kwa wachezaji hiyo huku siku chache kabla ya kuondoka wakijinoa pia kwenye upigaji wa mikwaju ya penati.

“Ninaiheshimu TP Mazembe kwa sababu ni timu kubwa yenye rekodi nzuri kwenye mashindano haya lakini hatuiogopi.Tumejiandaa kama tulivyopanga na nina imani kuwa tunakwenda kukitekeleza kile ambacho tumekifanyia kazi kwenye mazoezi.

“Natambua umuhimu wa mashabiki wetu ambao walikuwa wakitupa nguvu kwenye michezo yetu ya nyumbani tunaenda ugenini ambako mazingira yatakuwa tofauti ila niwatoe woga kwa kusema tutapambana kusonga mbele.

“Inawezekana kuingia hatua ya nusu fainali. Tulitengeneza nafasi kwenye mchezo wa kwanza ila tulishindwa kuzitumia hivyo naamini kuwa hata kwenye mchezo huu wa ugenini tunaweza kutengeneza nafasi,” alisema Aussems

Ili Simba isonge mbele kwenye hatua ya nusu fainali, inahitaji ushindi kwenye mchezo huo au sare ya aina yoyote ya mabao.

Kama mchezo huo ukimalizika kwa suluhu kama ilivyokuwa mchezo wa kwanza jijini Dar es Salaam, Simba na TP Mazembe basi mshindi ataamuliwa kwa mikwaju ya penalti.

Aussems alisema mchezaji pekee ambaye atakosekana kwenye kikosi chake ni beki wa kati, Pascal Wawa ambaye ni majeruhi baada ya kuumia kwenye mchezo wa kwanza uliofanyika jijini Dar es Salaam.

“Nina wachezaji 24 kwenye kikosi changu hivyo ni rahisi pindi anapoumia mmoja nafasi yake kuzibwa na mwingine, nadhani mliona namna Juuko alivyoziba pengo lake kwenye mchezo wa kwanza,” alisema kocha huyo wa Mbelgiji.

Nahodha wa kikosi hicho, John Bocco alisema wapo kwenye hali nzuri na akatoa ahadi kwa wapenzi na mashabiki wa Simba kuwa lengo lao ni kutinga nusu fainali na sio kitu kingine.

“Tunaenda kupambana. Kushikamana kwetu kwenye mchezo uliopita kama wachezaji kutaendelea ili tuweke historia nyingine ya kutinga hatua ya nusu fainali.

“Kuna mashabiki wetu ambao walitamani kuwa nasi DR Congo lakini kutokana na sababu za kiuchumi pengine wamekwama niwaombe kitu kimoja watuombee ili kila kitu kiende kama tulivyopanga,” alisema Bocco.

Katika mchezo huo Simba itawategemea zaidi wachezaji wake wanne ambao wana mabao mengi katika mashindano hayo wakiongozwa na Meddie Kagere mwenye mabao sita, Clatous Chama(5),John Bocco (3) na Emmanuel Okwi mwenye mabao mawili katika safu ya ushambuliaji.

Wapinzani woa TP Mazembe wanawategemea Tressor Mputu mwenye mabao manne sawa na Jackosn Muleka, Kelvin Mondeko mwenye mabao matatu na Meshack Elia aliyefunga mawili.

Kikosi kamili cha wachezaji wa Simba ambacho kimekwenda DR Congo ni Aishi Manula, Deogratius Munishi ‘Dida’, Zana Coulibaly, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Juuko Murshid, Erasto Nyoni, Paul Bukaba, James Kotei, Jonas Mkude.

Nyota wengine ni Mzamiru Yassin, Said Ndemla, Haruna Niyonzima, Hassan Dilunga, Clatous Chama, John Bocco, Meddie Kagere, Emmanuel Okwi na Rashid Juma.