Ushindi Simba kwa Songo uko hapa

Dar es Salaam. Wakati Simba ikijiandaa kuikabili UD Songo ya Msumbuji katika Ligi ya Mabingwa Afrika, wachezaji wa viungo wana nafasi kubwa ya kuibeba katika mchezo huo wa Jumapili wiki hii.

Simba itakuwa mwenyeji wa UD Songo ya Msumbiji katika mchezo wa marudiano wa Ligi ya Mabingwa Afrika kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam baada ya kutoka suluhu jijini Maputo.

Ingawa Simba itamkosa nahodha John Bocco ambaye ni majeruhi, safu ya kiungo inayoundwa na Clatous Chama, Sharaf Shiboub, Francis Kahata, Jonas Mkude, Mzamiru Yassin na Hassani Dilunga imebeba matumaini ya Watanzania katika mchezo huo.

Katika mechi tatu za hivi karibuni ilizocheza Simba dhidi ya UD Songo, Power Dynamos ya Zambia na Azam, viungo wa timu hiyo walicheza kwa kiwango bora kulinganisha na idara za ulinzi na ushambuliaji.

Katika mchezo dhidi ya UD Songo, Kocha Patrick Aussems alijaza idadi kubwa ya viungo kwa lengo la kucheza soka ya kujilinda jambo ambalo alifanikiwa.

Pia Simba ilipocheza na Power Dynamos, Aussems alijiachia kwa kucheza soka ya kufunguka huku akijaza wachezaji wa viungo walioipa Simba ushindi wa mabao 3-1.

Ubora wa Simba katika eneo hilo ulijidhihirisha dhidi ya Azam, kiwango bora cha safu ya kiungo kiliipa timu hiyo ushindi wa mabao 4-2 huku Shiboub akifunga mawili.

Mbali na Shiboub, nyota ya Chama inaonekana kung’ara zaidi Simba ikiwa nyumbani na hilo lilithibitika katika mechi za Ligi ya Mabingwa Afrika msimu uliopita.

Kiungo huyo wa kimataifa wa Zambia, alifunga mabao matano ambayo yaliiwezesha Simba kufuzu robo fainali.

Chama alifunga bao la tatu lililoipeleka Simba hatua ya makundi baada ya kuichapa Nkana Red Devils ya Zambia mabao 3-1. Ugenini timu hiyo ililala 2-1.

Pia aliipeleka Simba robo fainali baada ya kufunga bao la ushindi dakika ya 89 na kuiongoza Simba kuifunga AS Vita ya Congo mabao 2-1 jijini Machi 17.

Chama alifunga mabao matatu katika mechi za kirafiki Simba ilipoweka kambi Afrika Kusini, pia alifunga bao dhidi ya Power Dynamo ya Zambia kabla ya kufanya hivyo na Azam.

Shiboub anaonekana kuvaa viatu vya James Kotei baada ya kumiliki vyema eneo la kiungo. Mkenya Kahata ambaye ameifungia Simba bao moja ni hodari langoni mwa adui kutokana na kasi yake uwanjani.

Dilunga ambaye amekuwa akitokea benchi, ni mchezaji mwenye uwezo wa kubadili sura ya mchezo wakati wowote.

Kauli za wadau

Mchambuzi Ally Mayay alisema Simba msimu huu inabebwa na idadi kubwa ya wachezaji wa kiungo ambao wameonyesha nidhamu katika mechi zote walizocheza.

“Mfumo wa 4-3-3 inaotumia Simba unatoa nafasi kwa wachezaji wote wakiwemo washambuliaji kucheza kwa kasi kwasababu wanalishwa mipira na viungo.

“Kwa mfano Chama, Shiboub wote wanafunga hiyo itawasaidia kufanya vizuri katika mchezo wa Jumapili hata kama Bocco atakosekana,” alisema nahodha huyo wa zamani wa Yanga.

Kocha Kenny Mwaisabula alisema safu ya kiungo ndio mhimili wa timu katika mechi za mashindano, hivyo uwezo wa akina Chama utaisaidia Simba kucheza soka ya kufunguka kwa kuwa inahitaji ushindi.