VIDEO: Kocha Masoud kimenuka Msimbazi

Sunday October 7 2018

 

By Oliver Albert,Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Kauli ya Kaimu Rais wa Simba, Salim Abdallah ’Try Again’ inahitimisha mwisho wa kocha msaidizi, Masoud Djuma katika klabu hiyo ya Msimbazi.

Try Again amekiri kuwa hali ilipofikia ni mbaya kwa makocha Masoud na Patrick Aussems hivyo lolote linaweza kutokea.

Akizungumza na Azam Tv jana asubuhi, Try Again alisema kwa hali ya kutoelewana baina ya makocha hao ni ngumu kuendelea kukaa pamoja na kufika mbali.

“Tatizo la Masoud halijaanza leo, muda mrefu alikuwa haelewani na makocha wote waliokuwa juu yake, Joseph Omog, akaja Pierre Lechantre na sasa Aussems, tumejaribu sana kuliweka sawa jambo hilo lakini tunaona kadri muda unavyoendelea hali inakuwa ngumu zaidi.

“Ukweli ni kwamba sisi viongozi hatuna tatizo naye lakini hana maelewano mazuri na kocha mkuu na tumejaribu kuweka mambo vizuri lakini bado tunaona inakuwa ngumu,” alisema Try Again.

Aliongeza: “Siwezi kusema anabaki au anaondoka kwani bado ni mapema lakini lolote linaweza kutokea kuanzia sasa.”

Try Again alisema wao kama viongozi wanataka klabu hiyo iwe na umoja kuanzia kwa mashabiki, wachezaji na makocha.

Hata alipopigiwa kuhusu mkataba wake, Try Again alikataa kuweka wazi moja kwa moja na kusema: “Mtaelezwa kwa kuwa mkataba ni suala la mtu binafsi na mwajiri wake.”

Habari zinadai mechi dhidi ya Yanga iliyofanyika Septemba 30 ndiyo ilikuwa ya mwisho kwa kocha huyo Mrundi kukaa benchi la Simba na ilikuwa inasubiriwa kauli ya Bilionea wa klabu hiyo Moammed Dewji’ MO’ ndio afanye uamuzi wa mwisho.

Juzi MO alikutana na Djuma kwa saa mbili wakijadili kuhusu mkataba wa kocha huyo unaoelekea ukingoni. Hata hivyo, haikuwekwa bayana nini hasa kimezungumzwa.

Kocha huyo aliajiriwa na Simba Oktoba mwaka jana kama kocha msaidizi akichukua mikoba ya Mganda Jackson Mayanja aliyejiuzulu.

Djuma alikuwa akifanya kazi chini ya Mcameroon, Joseph Omog ambaye naye alifungashiwa virago Desemba mwaka jana baada ya Simba kuondolewa kwa mikwaju ya penalti na Green Warriors katika mashindano ya Kombe la Shirikisho (FA).

Siku chache baada ya Omog kutimuliwa, Djuma akapewa mikoba ya kuisimamia Simba na kibarua chake cha kwanza kilikuwa Kombe la Mapinduzi ambalo walitolewa hatua ya makundi na Azam FC.

Baada ya Mapinduzi Simba ikaleta kocha mkuu, Mfaransa, Pierre Lechante Januari mwaka huu ambaye aliingoza timu hiyo kutwaa ubingwa na kufuta ukame wa miaka mitano.

Hata hivyo, Lechante alidumu ndani ya klabu hiyo kwa miezi mitano tu kwani Juni mwaka huu aliondoka huku ikidaiwa alikuwa haelewani na Masoud na yeye wakati akiondoka alikiri hilo.

Baada ya Lechante kuondoka Simba ikamuajiri Mbelgiji,Patrick Aussems aliyepo hadi sasa.

Kwa nini anaondoka.

Habari zinadai kuwa Djuma ambaye alikuwa kocha bora Ligi ya Rwanda mwaka 2016 amekuwa akiingia katika migogoro na makocha wakuu jambo ambalo linapunguza ufanisi ndani ya timu.

Inadaiwa Djuma anataka kuwa kocha mkuu kwani anaona anastahili na si kuendelea kuwa msaidizi na ndio maana jambo hilo linamuumiza sana.

Inadaiwa kocha huyo amekuwa mtovu wa nidhamu licha ya kwamba mashabiki nje hawafahamu na kuendelea kuwa kipenzi chao.

Kutokana na kuingia katika mgogoro na kocha mkuu Aussems uongozi uliamua Djuma asijumuishwe katika safari tatu za mkoani walipokwenda kucheza na Ndanda Septemba 15 Mtwara na dhidi ya Mbao Septemba 20 na Mwadui uliofanyika Septemba 22.

Habari zaidi zinadai ilikuwa muda mrefu Djuma atimuliwe lakini viongozi walikuwa wakisubiri uamuzi wa mwisho kutoka kwa tajiri Mohammed Dewji’ Mo’ ambaye naye inasemekana ameridhia kwa mikono miwili kocha huyo aondoke ili asiendelee kuigawa timu hiyo.

Gazeti hili jana liliwasiliana na Djuma ili kuthibitisha madai ya kupewa mkono wa kwaheri alijibu kwa ufupi: ”No Coment! hivi sasa sizungumzi masuala yahusuyo timu.”

Naye kocha wa zamani wa timu ya Taifa ya Tanzania’Taifa Stars’ Dk Mshindo Msola alisema kama viongozi wameamua kumuondoa kocha huyo basi wamefanya uamuzi sahihi.

“Djuma anaweza kuwa kocha mzuri lakini nafikiri ana matatizo kwani haiwezekani asielewane na makocha wote watatu aliowahi kufanya nao kazi.

“Ukianza na Omog, Lechante ambaye alisema wazi kuwa Djuma ndio sababu ya yeye kuondoka na sasa Aussems. Nafikiri anataka kuwa kocha mkuu kwani anaamini anaweza sasa hapo ndipo tatizo linapoanza.

“Kama viongozi wanamuondoa ni jambo sahihi watakuwa wamefanya ili kuepusha matatizo zaidi kujitokeza na nadhani jambo hilo haliwezi kuwapa athari wachezaji kama viongozi watakaa na kuwaambia ukweli”alisema Msola.

Advertisement