Vigogo Yanga, Simba wakabana koo

Arusha. Matokeo ya Simba dhidi ya Al Ahly ya Misri, katika mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika, imewaibua watani wao wa jadi Yanga.

Simba juzi iliweka hai matumaini ya kucheza robo fainali, baada ya kuilaza Al Ahly bao 1-0, lililofungwa na Meddie Kagere kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Akizungumza mjini hapa jana, Katibu wa Yanga Tawi la Arusha Dietrich Kateule alisema hawatishwi na kiwango cha Simba katika mechi yao ya keshokutwa.

Alisema Yanga ina wachezaji hodari wa kuwadhibiti wachezaji wa Simba katika mechi yao ya Ligi Kuu Tanzania Bara.

“Hatuna wasiwasi hata kama jana (juzi) ameshinda hatuna hofu, kiwango chao tumekiona cha kawaida. Yanga ina wachezaji hodari wanaoweza kuipa timu matokeo mazuri,” alisema Kateule.

Mwenyekiti wa Simba Tawi la Arusha, Thabit Ustadh alidai tayari wamejiandaa kwenda Dar es Salaam kushangilia ushindi wa timu yao dhidi ya Yanga.

Ustadh alisema Simba ina nafasi ya kushinda mchezo huo kwa kuwa ina kikosi imara cha ushindi na alitoa mfano katika mechi ya juzi dhidi ya Al Ahly.

“Mechi ya awali tulitoka suluhu kutokana na baadhi ya matatizo yaliyokuwepo kipindi hicho, lakini Yanga isitarajie kupata hata pointi moja katika mechi yetu,” alisema mwenyekiti huyo.

Yanga inaongoza kwa pointi 58 Simba ina pointi 36 katika msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara.