Vigogo Yanga waanza na Ajibu

Muktasari:

  • Kamati ya klabu ya Yanga ipo mbioni kumuopngeza mkataba Nahodha wa timu hiyo Ibrahim Ajibu baada ya kusikia hesabu za watani wao Simba kuanza kumpigia hesabu mshambuliaji wao wa zamani kumrudisha kundini.

YANGA jana imepigwa bao 1-0 na Simba, lakini mapema ilishtukia jambo moja baada ya kusikia hesabu za watani wao kuanza kumpigia hesabu mshambuliaji wao wa zamani, Ibrahim Ajibu ili kumrudisha kundini, lakini vigogo wa Jangwani fasta wakafungua majadiliano ya mkataba mpya.

Mkataba wa Nahodha huyo wa Yanga, ambaye jana hakumaliza pambano la watani baada ya kutolewa dakika ya 61 ili kumpisha Mohammed Issa ‘MO Banka’ unafikia tamati mwishoni mwa msimu huu, lakini takwimu zinaonyesha kiwango alichokionyesha hadi kimewachanganya mabosi wa klabu hiyo na kuamua kumbakisha Jangwani.

Kocha Mwinyi Zahera, mapema aliliambia Mwanaspoti anatamani kubaki na Ajibu zaidi kutokana na kiwango alichokikubali kutoka kwa fundi huyo wa kujua kuuchezea mpira.

Kauli hiyo ya Zahera kumbe imeshatua kwa mabosi wa Yanga ambao tayari wameshakutana na meneja wa mchezaji huyo kuanza mazungumzo.

Taarifa kutoka ndani ya Yanga ni kwamba tayari mabosi hao wamekutana na meneja wa Ajibu wiki iliyopita kuanza mazungumzo hayo.

“Tumeanza kufanyia kazi mahitaji ya kocha na kwa umuhimu wake tayari tumeanza na nahodha katika kumbakiza kwa kuwa kocha anamhitaji zaidi,” alisema bosi huyo.

“Mchezaji mwenyewe alikuwa kambini, hivyo tumekutana na meneja wake tumemweleza dhamira yetu sasa akikutana na mchezaji wake watatuambia kinachohitajika kwa upande wao.

Katika misimu miwili aliyoichezea Yanga kitokea Msimbazi, Ajibu amefunga mabao 13, saba ya msimu uliopita na sita aliyotupia kambani mpaka sasa, huku akiwa ndiye kinara wa asisti katioka Ligi Kuu Bara akisaidia kupatikana kwa mabao 14 akiiweka Yanga kileleni ikiwa na alama 58.

Ajibu na Amissi Tambwe ndio wachezaji wanaofuata kwa mabao mengi ndani ya Yanga msimu huu wakiongozwa na Heritier Makambo mwenye mabao 11 akiongoza orodha ya Ligi Kuu Bara sambamba na Salum Aiyee wa Mwadui aliongea idadi hiyo juzi wakati timu yake ikiitambia Coastal Union kwa mabao 2-1 mjini Shinyanga.