Visa vya VAR na ladha ya soka

Tangu ilipoanza kutumika teknolojia ya usaidizi wa video kwa waamuzi ‘VAR’ katika mashindano mbalimbali msimu uliopita, imekuwa gumzo duniani kote.

Visa vya VAR vinajulikana kuanzia kwenye Kombe la Dunia mwaka jana nchini Urusi hadi Ligi ya Mabingwa Ulaya na hata Afrika. Pia zipo baadhi ya ligi ambazo zilianza kutumia teknolojia hiyo msimu uliopita.

Wapo wanaosema inatenda haki kwenye matukio mbalimbali ambayo kabla ya hapo yalikuwa sio rahisi kuonwa na waamuzi.

Mtazamo mwingine ni kwamba VAR imekuja kupunguza umakini wa waamuzi uwanjani na wakati mwingine wanafanya uamuzi ambao si sahihi kitu ambacho kinapunguza ladha ya mchezo.

Yafuatayo ni baadhi ya matukio yenye utata ambayo yamejitokeza katika Ligi Kuu England (EPL) na kuamuliwa na VAR huku yakiacha maswali mengi kwa wadau wa soka.

Manchester City 2-2 Tottenham Hotspurs

Mechi hii ilikuwa ya mzunguko wa pili ambapo ndani ya dimba la Etihad, Manchester City waliwakaribisha Tottenham Hotspurs. Hiyo ilikuwa ni Agosti 17.

Baada ya piga nikupige timu hizo zilifika kwenye dakika za majeruhi matokeo yakiwa ni 2-2. Katika sekunde za mwisho Man City walihisi kunyakua alama zote tatu baada ya Gabriel Jesus kuukwamisha mpira wavuni.

Wakati wachezaji wa Man City pamoja na benchi la ufundi sambamba na mashabiki wakiwa kwenye dimbwi la furaha, mwamuzi Michael Oliver alitonywa kuhusu tukio la kabla ya bao kufungwa.

Mwamuzi aliambiwa kuwa Aymeric Laporte ambaye ni mlinzi wa Man City aliunawa mpira kabla ya kufika kwa mfungaji, na hivyo kuhakikishiwa kuhusu suala hilo alilifuta bao hilo na mechi ikaisha kwa 2-2. Hilo ndilo lilikuwa tukio la kwanza kubwa la kusisimua msimu huu ambalo mashabiki wa soka England walilishuhudia.

Hata hivyo, kwenye tukio hilo uamuzi ulikuwa ni sahihi hasa ukizingatia sheria mpya ya kunawa mpira ndani ya boksi.

Arsenal 2-2 Crystal Palace

Mechi ya Novemba 2 ambapo Arsenal walikuwa nyumbani kuialika Crystal Palace. Kwenye wiki hiyo EPL ilishuhudia matukio mengi yakiamuliwa na VAR.

Ndani ya mechi hii tu Crystal Palace walizawadiwa penati ambayo ilitokana na VAR, lakini tukio kubwa zaidi lilikuwa katika dakika za majeruhi ambapo mlinzi wa Arsenal, Sokratis Papastathipoulos alidhani amefanikiwa kuipa timu yake bao la tatu na la ushindi kwenye mchezo huo.

Bao hilo alifunga kwa kichwa na baada ya kushangilia kwa muda mrefu mwamuzi alilifuta kwa madai kuwa mchezaji wa Arsenal, Collum Chambers alimfanyia madhambi Gary Cahil wa Palace kabla ya kufungwa, hivyo bao likafutwa na mechi ikaisha kwa mabao 2-2.

Uamuzi huo ulikuwa na utata hasa yakiangaliwa kwa makini ‘madhambi’ aliyochezewa Cahil.

Liverpool 3-1 Manchester City

Ilikuwa ni mechi ya Novemba 10 ambayo imeacha maswali mengi. Mechi hiyo ambayo ilikuwa ni ya wapinzani wawili kwenye mbio za ubingwa ilishuhudia mwamuzi Michael Oliver akishindwa kuomba usaidizi wa VAR licha ya kuwa ilionekana dhahiri kulikuwa na matukio hasi.

Tukio kubwa ni lile la mlinzi wa pembeni wa Liverpool, Alexander Anorld kuonekana kuushika mpira ndani ya boksi akijaribu kuzuia krosi iliyopigwa na Raheem Sterling.

Ukiangalia aina ya penati ambazo zimekuwa zikitolewa kwa timu mbalimbali tangu VAR ilipoanza kufanya kazi huwezi kuona ni namna gani City wangenyimwa penati katika tukio hilo.

Hata hivyo, Oliver hakuona na hata watu waliokuwa kwenye ‘monita’ za VAR hawakutaka kuangalia licha ya kuwa kocha Pep Guardiola wa City na wachezaji wake walilalamikia tukio hilo.

Tottenham Hotspurs 1-1

Sheffield United

Mechi ya Novemba 10 ambayo iliwakutanisha wenyeji Spurs dhidi ya Sheffield United. Mechi hiyo iliisha kwa timu hizo kufungana bao 1-1. Hata hivyo, Shefield wanahisi pengine wangepata alama zote tatu kama sio bao lao kukataliwa kwa utata kutokana na madai ya mchezaji wao kuotea.

Mshambuliaji David McGoldrick alifunga bao safi, lakini kwa mujibu wa VAR wakati wa kutengeneza bao hilo, Enda Steven alikuwa akipokea pasi ambayo nayo aliipiga kati na kwenda kuzaa bao.

Hata hivyo picha nyingi za marudio zinaashiria utata mwingi uligubika tukio hilo kwani mistari iliyopigwa wakati wa kuangalia haionyeshi kama kweli Enda alikuwa ameotea, bali zinaonyesha Eric Dier ambaye ni mlinzi wa Spurs kuwa alikuwa mtu wa mwisho kabisa.

Brighton 3-2 Everton

Wakati zikiwa zimesalia dakika 10 mpira kwisha, Everton walikuwa mbele kwa mabao 2-1 katika mchezo huo wa Oktoba 26. Kwenye dakika ya 80, kupita VAR, Brighton walizawadiwa penati kwa madai kuwa Michael Keana alimgonga mshambuliaji wao Aaron Connolly kwa nyuma.

Hata hivyo, picha za marudio hazionyesha madai hayo na hilo ni mojawapo kati ya matukio ambayo mtandao wa ‘Game on news’ kupitia kitengo chake cha VAR wamekuwa na kawaida ya kupitia matukio mbalimbali na kisha kuyatolea ufafanuzi, wanaulalamikia.

Kwenye tukio la penati ya Brighton, kwa mujibu wa taarifa iliyotelewa mara baada ya mchezo huo ni kwamba Everton walionewa.