#WC2018: Deschamps apiga mkwara kikosi cha Ufaransa

Sunday July 15 2018

 

Moscow, Russia. Kuelekea mchezo wa kukata na shoka wa fainali ya makala ya 21 ya Kombe la Dunia, Kocha wa Ufaransa amewataka wachezaji wake kupunguza mchecheto na kuwa na utulivu mkubwa kabla na wakati wa mechi hiyo, kama wanataka ushindi.

Baada ya kuiongoza Les Blues, kutwaa ubingwa huo mwaka 1998, akiwa nahodha, Deschamps anaonekana kuwa na uzoefu mkubwa wa kuhimili presha ya mechi ya fainali na ili kufanya hivyo, amewataka akina Mbappe, Pogba, Griezmann na wengineo kutuliza mzuka.

"Ni fahari kubwa kusimama kati ya mataifa 32 na kutawazwa bingwa, ni fahari kucheza fainali, mwaka 1998 tulifanya hivyo, mwaka huu tunataka kufanya hivyo, lakini kama hatutakuwa na utulivu kabla na ndani ya uwanja itakuwa ngumu kufanikisha ndoto yetu. Tunatakiwa kutulia na kucheza kwa utulivu mkubwa," alisema Deschamps.

 

 

Kocha huyo anayetarajia kuweka rekodi ya kuwa mfaransa wa kwanza kuwahi kutwaa kombe la Jules Rimet akiwa mchezaji na Kocha akiungana na wababe Mario Zagallo wa Brazil na Mjerumani Franz  Beckenbauer, anaamini kama hawatotulia mchezoni, itakuwa ngumu kuwafunga Croatia.

Croatia wanacheza fainali yao ya kwanza ya Kombe la Dunia, ambapo watakuwa na kila sababu ya kupambana na kutokana na kikosi kizuri walichonacho akiwemo nahodha Luca Modric na Ivan Rakitic.

Kwa upande wao, France wataingia Luzhniki wakiwa na hamu ya kutwaa taji lao la pili huku wakitaka kutokurudia makosa waliofanya kwenye mchezo wa fainali ya Euro 2016, walipofungwa na Ureno. Yote tisa, kumi tukutane Luzhniki.

Advertisement