#WC2018: Fainali ya Giroud, Mandzukic

Muktasari:

  • Majina haya ni ya washambuliaji watakaoziongoza timu zote mbili, lakini hayatajwi sana wala kupewa nafasi na wengi isipokua makocha n ahata wachezaji wenzao wanajua thamani na umuhimu wao uwanjani.

Wengi hawajui kuwa kati ya vikosi viwili vitakavyoshuka dimbani leo katika mechi ya fainali ya Kombe la Dunia, yapo majina mawili makubwa yasiyofahamika na wengi.

Majina haya ni ya washambuliaji watakaoziongoza timu zote mbili, lakini hayatajwi sana wala kupewa nafasi na wengi isipokua makocha n ahata wachezaji wenzao wanajua thamani na umuhimu wao uwanjani.

Hao ni washambuliaji viongozi wa mashambulizi yaani namba 9. Olivier Giroud wa Ufaransa na Mario Mandzukic wa Croatia.

Jamaa hawa ndio wachezaji wakongwe ‘zilipendwa’ kuliko wote katika vikosi vyao na yamkini wamecheza muda mrefu katika vikosi na mechi nyingi pia.

Giroud mwenye miaka 31 ndiye ‘mtu mzima’ kwenye kikosi cha Ufaransa, alianza kuitumikia mwaka 2011 tayari amecheza mechi 80 na kufunga mabao 31.

Mandzukic ana miaka 32, ndiye ‘babu’ kwenye kikosi cha Croatia, amecheza mechi nyingi kuliko wenzake wote watakaoshuka dimbani kuipigania nchi yao, amecheza mechi 88, kufunga mabao 32 tangu alipoanza kucheza mwaka 2007.

Katika fainali hizi Giroud hajafunga licha ya kuchea mechi zote lakini mchango wake umeendelea kuwa muhimu kwa timu, wakati Mandzukic, ameshazifumania nyavu na mchango wake umesaidia kuifikisha Croatia fainali.