#WC2018: Mfanya usafi na Fundi umeme uso kwa uso Kombe la Dunia

Tuesday June 19 2018

 

Moscow, Russia. Macho na masikio yataelekezwa katika uwanja wa Luzhniki, wenye uwezo wa kuingiza mashabiki wapatao 80,000, kwa ajili ya kushuhudia mchezo wa kukata na shoka wa kundi B, kati ya Ureno na Morocco. Utakuwa ni vita ya mafahali wawili, kila mmoja akihitaji ushindi.

Wakati kila mmoja akitamani kushuhudia mambo ya Cristiano Ronaldo baada ya kupiga hat-trick katika mechi ya kwanza dhidi ya Hispania, ulimwengu wa soka utashuhudia mafahali wawili wakikutana pale Moscow. Nawazungumzia makocha wawili, Herve Renard wa Morocco na mwenzake, Fernando Santos wa Ureno.

JE UNAJUA....

Mbali na rekodi ya makocha hawa katika ulimwengu wa soka, kuna siri nzito nyuma ya pazia katika maisha ya makocha hao. Ni hivi, kesho, kuanzia saa tisa alasiri, kwa mara ya kwanza, kwenye michuano hii ya kombe la Dunia, mashabiki watashuhudia Fundi Umeme na Mfanya usafi wa zamani, wakiongoza timu zao kusaka pointi tatu muhimu.

Kabla ya kutusua katika soka, Herve Renard aliwahi kufanya kazi nyingine ya kumuingizia kipato, kazi ni kazi wanasema unashangaa? Wakati huo, kabla ya kujulikana, kabla ya kuiongoza Zambia kwa mafanikio makubwa miaka 10 iliyopita, Renard alikuwa ni muokota makopo, kwa lugha ya stara, mfanya usafi.

Renard, ambaye alipoteza mchezo wa kwanza dhidi ya Iran, inasemekana akiwa na umri wa miaka 15, alifanya majaribio katika klabu ya Cannes, akiwa na matumaini ya kupata mafanikio, lakini kwa bahati mbaya mambo yalimuendea kombo.

Baada ya kujikuta akiwa mchezaji wa levo ya tatu katika kikosi, Renard, aliamua kujaribu maisha kwa mlango mwengine, akafungua kampuni ya kuokota uchafu 'makopo' mitaani na kulipwa ujira ambao aliutumia kuendeshea maisha. Alikuwa mfanya usafi. Kazi hii aliifanya usiku mnene.

“Huwa nakumbuka maisha yangu ya nyuma, nakumbuka miaka ile ya tabu, nilikuwa naamka usiku wa manane kwa ajili ya kwenda kuokota taka, kazi yetu ilikuwa ni kusafisha mji kabla watu hawajaamka, ilikuwa ni kazi ngumu, lakini ukiwa mjini hakuna kuchagua," alisema Renard.

Lakini, licha ya kufanya kazi, huku ndoto ya kugeza mpira wa kulipwa ikiwa imefutika, Renard alianza kufundisha timu za mchangani, kabla ya nyota yake kumkuna Kocha mzoefu, Claude Le Roy, ambaye alimchukua na kumfanya msaidizi wake.

Hapo ndipo ukawa mwanzo wa Renard mwenye mashati meupe, huo ndio ukawa mwanzo wa mwendelezo wa uwezo wa Renard. Renard aliiongoza Zambia kushinda taji lao la kwanza la Kombe la Maabara Afrika mwaka 2012. Miaka mitatu baadaye akaiongoza Ivory Coast kubeba ubingwa wa Afrika.

Hivi sasa yuko Russia akiiongoza Morocco, ambayo ameisaidia kushiriki michuano ya kombe la dunia baada kukosa tiketi hiyo kwa zaidi ya miaka 20. Huyu ndio Herve Renard, mwokota makopo mbishi aliyeliteka soka la Afrika.

Fernando Santos, katika moja ya mahojiano na waandishi wa habari mwaka jana, alisema kabla ya kuwa kocha maarufu, amewahi kufanya kazi kama fundi umeme katika moja ya hoteli maarufu, nchini mwake.

Ni kwamba, Santos ambaye ana taaluma ya Umeme, uhandisi qa Umeme, alianza kufanya kazi kama mkuu wa kitengo cha ufundi (chief Technician), ambapo kwa mujibu wa kauli take mwenyewe, hakuwa na lengo la kuendelea na soka kabisa.

Hata hivyo, wakati akiwa amwshakata shauri ya kutojihusisha na maswala ya soka, mwajiri wake, wakati huo, ambaye alikuwa ni Rais wa timu ya daraja la pili ya Estoril, alimuomba kuchukua mikoba ya kuionoa klabu hiyo kwa muda.

“Nikiwa nafanya kazi katika ile hoteli kama fundi umeme, mwajiri wangu aliniomba nifundishe klabu ya Estoril, aliyokuwa anaimiliki kwa muda wa mwezi sita, lakini badala ya miezi nilidumu na klabu hiyo kwa miaka sita. Tukafanikiwa kupanda daraja," alisema Santos.

Baada ya kuacha kazi katika klabu hiyo, Santos alifanikiwa kufanya kazi katika klabu tatu kubwa za Ureno, ambazo ni Benfica, Sporting na Porto, kabla ya kuliongoza taifa la Ugiriki, kwenye michuano ya Kombe la Dunia mwaka 2014. Lakini Kocha alikuja kuishtua dunia alipoiongoza Ureno kutwaa ubingwa wa Euro 2016.

Advertisement