#WC2018: Shearer amvulia kofia kocha Southgate

Muktasari:

  • Shearer amemwamgia sifa mlinzi wa Leicester City, Harry Maguire, akisema ndiye alikuwa mhimili wa England katika fainali za Kombe la Dunia 2018, licha ya England kung’olewa katika nusu fainali, anastahili pongezi.

Moscow, Russia. Nahodha wa zamani wa England, Alan Shearer amemvulia kofia kocha Gareth Southgate kwa kuwaamini wachezaji wasio na majina ambao wamefanya mambo makubwa katika fainali za mwaka huu za Kombe la Dunia.

Shearer amemwamgia sifa mlinzi wa Leicester City, Harry Maguire, akisema ndiye alikuwa mhimili wa England katika fainali za Kombe la Dunia 2018, licha ya England kung’olewa katika nusu fainali, anastahili pongezi.

Alimpongeza Kocha Southgate kuwaamini wachezaji wasio na majina makubwa na kuwaacha wale wenye majina mfano kipa Joe Hart, kiungo Jack Wilshere na wengine, akisema tofauti na miaka iliyopita kikosi cha mwaka huu kimefanya makubwa.

“Sijali timu kutolewa katika nusu fainali, lakini nampongeza Kocha Southgate kuwaamini kwake wachezaji wasio na majina makubwa kumetusaidia kupiga hatua, hakuna aliyetarajia kipa Jordan Pickford au mlinzi Harry Maguire wangefanya kazi nzuri hivi, kweli nampongeza kwa dhati kocha vijana hawajatuangusha,” alisema.

Shujaa huyo wa zamani wa England, alifichua kuwa alifurahia kuona Maguire akicheza kwa kujiamini na kujitolea kwa ajili ya Taifa, akiwawadhibiti wachezaji mahiri na kuufanya ukuta wa England kutopitika kirahisi.

“Narudia ingawa England imetolewa, binafsi nampongeza kocha pamoja na wachezaji wote, Harry Maguire, amefanya kazi kubwa natamani kuona analinda kiwango chake,” aliandika kwenye mtandao wake wa kijamii wa Twitter.