Waarabu CAF waitega Simba

MABOSI wa Simba mpaka sasa wapo kimya kwenye ishu zao za usajili, ikielezwa mambo mawili ndio yanayowabana, lakini unaambiwa wawakilishi hao wa Tanzania katika Ligi ya Mabingwa Afrika wamejikuta wakiwa katikati ya mtego wa Waarabu wa CAF.

Sio Simba tu, hata watani zao Yanga nao wamewekwa mtu kati ya Waarabu hao ambao wamekuwa wakitawala soka la Afrika wakigawana tu mataji ya michuano ya CAF kila msimu na kuzifanya klabu nyingine shiriki kuonekana kama za kawaida tu.

Ni hivi. Tanzania kwa mara ya kwanza msimu ujao wa michuano ya CAF itawakilishwa na klabu nne, zikiwamo Simba na Yanga zitakazocheza Ligi ya Mabingwa Afrika na KMC na Azam zitakazokinukisha kwenye Kombe la Shirikisho Afrika msimu wa 2019-2020.

Matumaini makubwa ya wadau ya soka wameyawekwa kwa Simba ambayo msimu uliopita wa michuano hiyo ya CAF walifika robo fainali na kuibeba Tanzania, lakini pia wakizipa nafasi pia Yanga na Azam ambazo zina uzoefu wa michuano hiyo ya Afrika.

Hata hivyo, katikati ya tumaini hilo la wadau wa soka wa Tanzania, ni wazi vigogo hivyo lazima vijipange kwelikweli msimu ujao kwani wasipofanyaa hivyo huenda hata hatua ya makundi waisikie tu hewani kutokana na mtego waliowekewa na Waarabu.

Kitendo cha kufuzu kwa klabu 13 kutoka Afrika ya Kaskaini katika michuano hiyo ya Ligi ya Mabingwa, imekuwa ni kama mtego kwa Simba na Yanga katika kupenya kushiriki michuano hiyo inayoanza Agosti mwaka huu hadi Mei mwakani itakapofikia tamati.

Idadi hiyo ya vigogo vya soka inaweza kuongezeka zaidi mara baada ya baadhi ya ligi za nchi kumalizika na kuzidi kuzipa presha Simba na Yanga kwenye mashindano hayo.

Kundi hilo la timu 13 ambazo majina yake yake yanaweza kuzitikisa Simba na Yanga, linajumuisha zile ambazo zimewahi kutwaa ubingwa wa Afrika kwa nyakati tofauti, zile ambazo zina uzoefu na mashindano hayo pamoja na zile ambazo zimekuwa zikifanya vizuri katika siku za hivi karibuni huku zikiwa na uwekezaji mkubwa.

Mabingwa wa kihistoria wa Afrika, Al Ahly waliotwaa taji mara nane, wameshakata tiketi ya uwakilishi wa Misri, ikikumbukwa ni moja ya timu iliyokuwa kundi moja na Simba na kuifumua Msimbazi mabao 5-0 kwao kabla ya kulala ugenini jijini Dar kwa bao 1-0.

Mbali na Al Ahly, TP Mazembe ya DR Congo inayoshika nafasi ya pili kwa kutwaa taji hilo mara nyingi ikibeba matano na iliyoing’oa Simba kwenye robo fainali kwa jumla ya mabao 4-1 nayo imepenya sambamba na AS Vita walioiaibisha Msimbazi mjini Kinshasa.

Vita iliifumua Simba mabao 5-0 katika mechi ya makundi, kabla ya kulala 2-1 jijini Dar katika mechi iliyojaa vibweka ikiwamo nyota wa timu hiyo ya DR Congo kuvaa maski kwa kisingizio cha kupuliziwa sumu na wenyeji wao. Kipigo hicho kiliivusha Simba robo fainali.

Wakongo hao wa Vita nao wamo kwani wameshalibeba taji hilo mara moja, lakini pia kuna Esperance ya Tunisia iliyotoka kubeba taji hivi karibuni katika fainali iliyobaki kuwa gumzo kwa kuvunjika baada ya Wydad Casablanca kugomea. Watunisi wamelibeba mara tatu kama ilivyo kwa Raja Casablanca ya Morocco ambao nao wamefuzu michuano ya msimu ujao ya Afrika sambamba na Wydad na JS Kabylie (Algeria) ambazo kila moja imechukua ubingwa mara mbili ubingwa wa Afrika.

Pia, kuna timu zilizobeba taji mara moja ambazo nazo zimefuzu ni Mamelodi Sundowns na Orlando Pirates za Afrika Kusini, hapo ni mbali na Zesco United ya Zambia na Horoya ya Guinea ambazo kwa misimu miwili iliyopita zilicheza hatua ya makundi ya mashindano ya klabu Afrika pamoja na 1º de Agosto ya Angola iliyocheza nusu fainali za 2018.

RAGE HANA PRESHA

Kitendo cha Simba na Yanga kufuzu kwa pamoja na kutarajiwa kukutana na vigogo hao sambamba na timu nyingine kabla ya kupangwa kwa droo ya michuano hiyo, kimemfanya aliyekuwa Mwenyekiti wa Simba, Ismail Aden Rage kufunguka.

Rage aliyewahi kuwa Katibu Mkuu wa TFF (enzi za FAT), alisema haoni kinachoweza kuwapa fresha wawakilishi hao wa Tanzania, maadam wajipange vizuri.

“Kitendo cha kuingiza timu nne kwenye mashindano ya Afrika ni jambo jema na linaonyesha soka letu linapiga hatua, hivyo jambo la msingi ni klabu zetu kujiandaa vyema ili zifanye vizuri,” alisema.

Rage aliongeza anaamini Simba inaweza kufanya maajabu kuliko ya msimu uliopita kama tu itasajili vyema na kujiandaa vyua kutosha kwenye michezo.

Rage alisema ni kweli kuna vigogo vinavyotetemesha klabu nyingine za Afrika, lakini zinafungika kama ambavyo Simba ilivyofanya msimu uliopita kwa kutofungwa nyumbani na Al Ahly, AS Vita, Nkana Red Devils na TP Mazembe, japo walienda kunyamazishwa ugenini.