Wachezaji Simba, Yanga watakaokuwa watazamaji

Muktasari:

  • Wachezaji hao wameachana na timu hizo na kwenda klabu nyingine tofauti.

Dar es Salaam. Timu kongwe za Ligi Kuu Bara za Simba na Yanga zinacheza kesho Jumamosi lakini wapo wachezaji ambao walikuwepo katika timu hizo lakini watakosekana.

Wachezaji hao wameachana na timu hizo na kwenda klabu nyingine tofauti.

Shiza Kichuya (Simba)

Winga wa zamani wa Simba, Shiza Kichuya ambaye ana historia ndani ya kikosi hicho pindi Wekundu hao wa Msimbazi wanapoivaa Yanga mara nyingi huwa anawafunga na alikuwepo katika mechi iliyopita ambayo ilimalizika kwa suluhu.

Kwa sasa Kichuya yuko nchini Misri anaichezea Klabu ya ENPPL baada ya Pharco ya nchini humo iliyomnunua kumtoa kwa mkopo.

Marcel Kaheza (Simba)

Mshambuliaji wa FC Leopard ya Kenya, Marcel Kaheza amejiunga na klabu hiyo katikati ya msimu huu akitokea Simba. Ni miongoni mwa mwachezaji waliokuwepo wakati Simba inacheza na Yanga mara ya mwisho hivyo ataangalia kama mtazamaji kideoni.

Mohammed Rashid 'Mo Rashid' (Simba)

Mshambuliaji wa zamani wa Simba, Mohammed Rashid 'Mo Rashid' kwa sasa anaichezea KMC baada ya kutolewa kwa mkopo klabuni hapo. Ni miongoni mwa wachezaji waliokuwepo Simba katika mechi iliyopita lakini alicheza.

Beno Kakolanya (Yanga)

Mlinda mlango wa Yanga, Beno Kakolanya aling'ara ndani ya kikosi hicho mchezo uliopita, lakini safari hii kama atabaki kuwa mtazamaji tu.

Kakolanya amezua hali ya sintofahamu ndani ya kikosi hicho jambo lilimfanya akae nje ya kikosi chake hicho cha Jangwani na inadaiwa ameanzisha biashara yake ya mchele ambayo inakwenda vizuri.

Yohana Mkomola (Yanga)

Mshambuliaji wa African Lyon, Yohana Mkomola ni miongoni mwa walioondoka Yanga katikati ya msimu na alikuwepo katika mechi iliyopita ya watani wao Simba.

Pato Ngonyani (Yanga)

Kiraka wa African Lyon mwenye uwezo wa kucheza nafasi nyingi uwanjani za ulinzi kama beki ya kulia, kati na kiungo. Alikuwepo katika mchezo wa Yanga na Simba uliopita lakini katikati ya msimu alitolewa kwa mkopo kwenda klabu hiyo iliyo chini ya bosi, Rahim Zamunda.

Yusuph Mhilu (Yanga)

Mshambuliaji aliyetikisa kwa muda ndani ya kikosi cha Yanga, lakini Kocha Mwinyi Zahera na mabosi wake waliamua kumtoa kwa mkopo aende African Lyon anayochezea sasa.

Alikuwepo wakati Yanga ilipocheza na Simba mara ya mwisho matokeo yakawa 0-0.