Wambura achomolewa Bodi ya Ligi

Dar es Salaam. Nafasi ya mtendaji mkuu wa Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB), imebaki wazi kufuatia uamuzi wa Shirikisho la Soka nchini (TFF) kutomuongezea mkataba Boniface Wambura.

Wambura amepewa nafasi mpya iliyoundwa na TFF ya mkurugenzi wa Idara ya Habari na Masoko ambayo ndani yake itakuwa na vitengo viwili huku shirikisho likitangaza kuanza mchakato wa kumsaka mrithi wake.

Gazeti la Mwanaspoti la Oktoba 12 liliripoti kuhusu mabadiliko ndani ya TFF na kuondolewa kwa Wambura katika nafasi ya mtendaji mkuu.

Wambura atakuwa mkurugenzi wa Idara ya Habari na Masoko ya TFF atasaidiwa na mkuu wa masoko, Aaron Nyanda; upande wa habari Clifford Ndimbo,” alisema Wilfred Kidao, katibu mkuu wa TFF.

“Kamati ya Utendaji iliyokutana hivi karibuni imeagiza kuanza mchakato wa kumsaka mtendaji mkuu wa Bodi nafasi ambayo itatangazwa kwenye vyombo vya habari.”

Wambura aliyeongoza Bodi ya Ligi kwa miaka minne tangu Juni 2015, anaondoka akiwa ameacha alama ya kuongeza thamani ya udhamini wa ligi kutoka Sh3 bilioni hadi Sh6 bilioni kwa msimu.

Pia TPLB iliongeza wadhamini wa Ligi Kuu, kutoka wawili Kampuni za Vodacom na Azam Media hadi watatu, ikiongezeka Benki ya KCB.

Pamoja na mafanikio hayo, TPLB ilishindwa kuondoa changamoto sugu kama vile mabadiliko ya mara kwa mara ya ratiba za ligi, uchakavu wa viwanja na waamuzi.

Mbali na Wambura, Kidao alisema mchakato wa mabadiliko ya Katiba ya TFF umesababisha kupunguzwa idadi ya wajumbe wa kamati ya utendaji na mkutano mkuu.

“Fifa Wametaka kupunguza ukubwa wa kamati ya utendaji. Wanaamini kunapokuwa na kamati kubwa kunapunguza ufanisi. Kikao cha Kamati ya Utendaji kinakutana mara nne kwa mwaka, lakini kwa mabadiliko haya kitakutana kila baada ya miezi miwili,” alisema Kidao.

Pia TFF imetangaza mkurugenzi mpya wa Ufundi, Oscar Mirambo kujaza nafasi Ammy Ninje ambaye mkataba wake ulivunjwa baada ya kumalizika Fainali za Mataifa ya Afrika (Afcon), zilizofanyika Misri kuanzia Juni 21 hadi Julai 19.

Mwenyekiti wa Bodi ya Ligi Tanzania (TPLB), Steven Mnguto alisema siyo tatizo kutangazwa mabadiliko ndani ya bodi wakati muda wa aliyekuwa akishika nafasi hiyo umemalizika. “Kulikuwa na mambo yanafanyika ndio maana hatukuona sababu ya kufanya maamuzi ya haraka, kwa sababu ilitupasa tukae na kuongea na aliyekuwa anashika nafasi hiyo,” alisema Mnguto.

Gazeti hili lilipohoji kwa nini nafasi hiyo isitangazwe na TPLB badala yake ikatangazwa na TFF, Mnguto alisema: “Bodi ya Ligi haina mamlaka kisheria na haijiamulii mambo yake, bado tupo chini ya TFF kwa hiyo hata wafanyakazi wa TPLB ni wafanyakazi wa TFF.”

Wambura alipotafutwa ili kujua namna alivyopokea mabadiliko hayo alisema yupo kwenye kikao.