Wambura awaibua El Maamry, Tandau

Thursday December 6 2018

 

By Imani Makongoro, Charles Abel [email protected]

Dar es Salaam. Mtazamo tofauti wa wadau kuhusiana na uamuzi wa Mahakama kutengua adhabu ya kifungo cha maisha kujihusisha na soka inayomkabili aliyekuwa Makamu wa Rais wa TFF, Michael Wambura, unaongeza sintofahamu.

Ijumaa, Novemba 30, Mahakama Kuu Tanzania ilitengua uamuzi wa Kamati ya Maadili ya Shirikisho la Soka Nchini (TFF) baada ya kubaini kuwa madai ya Wambura yana mashiko. Wambura alichukua uamuzi wa kufungua kesi mahakamani kupinga utaratibu uliotumika kumfungia akidai ulikuwa batili na haukufuata matakwa ya kisheria, kanuni na Katiba ya shirikisho hilo.

Hatua hiyo ilifuatia rufani ya Wambura kwa Kamati ya Rufani ya Maadili ya TFF chini ya Wakili Ebenezer Mshana kuitupilia mbali rufani ya kigogo huyo aliyoikata siku chache baada ya kupewa adhabu ya kifungo cha maisha kwa kukutwa na hatia ya makosa matatu ya kimaadili.

Makosa hayo kwa mujibu wa kamati hiyo ni kupokea/kuchukuwa fedha za TFF za malipo ambayo hayakuwa halali, kughushi barua ya kueleza alipwe malipo ya Kampuni ya Jekc System Limited huku akijua malipo hayo siyo halali na kosa jingine ni kufanya vitendo vinavyoshusha hadhi ya shirikisho. Kufuatia Wambura kwenda mahakamani na kushinda madai yake, swali kubwa ambalo kundi kubwa la wadau wa soka wamekuwa wakijiuliza kama uamuzi huo ulikuwa uhalali au vinginevyo.

Hoja hiyo imeibuka kutokana na dhana iliyojengeka muda mrefu kuwa Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa), haliungi mkono masuala ya mchezo huo kuamuliwa na vyombo vya nje ya mpira wa miguu kama mahakama na Serikali.

Uamuzi wa Fifa kuzuia kupeleka masuala ya soka mahakamani unalenga kupunguza migogoro ya mara kwa mara kwenye nchi na kuhakikisha kunakuwa na utulivu, shirikisho hilo linalazimisha uwepo wa kamati za kisheria ndani ya vyama au mashirikisho ya soka kwenye nchi husika. Sintofahamu hiyo imewafanya wadau kugawanyika kimtazamo wapo wanaoamini Wambura amefanya jambo sahihi kwenda mahakamani kudai haki yake na wengine wakiona alikosea kwa sababu masuala ya soka hayapelekwi mahakamani.

Mjumbe wa Heshima wa Shirikisho la Soka Afrika (CAF), Said El Maamry ambaye kitaaluma ni mwanasheria, alisema, suala la Wambura lina walakini, ingawa kwenda mahakamani ni haki yake ya msingi kwani sheria za nchi hazitambui kama FIFA hairuhusu masuala ya mpira kupelekwa Mahakamani.

“Hili suala TFF walipaswa kulimaliza wenyewe mapema kabla ya Wambura kufikia hatua ya kwenda mahakamani. Bahati mbaya haikuwa hivyo, lakini ‘rungu’ la Fifa itategemea na namna kesi hiyo ilivyo,” alisema Mzee El Maamry.

Mkufunzi wa FIFA nchini, Henry Tandau alisema suala la Wambura linategemeana na mazingira yake.

“Unajua hili suala inategemea Wambura alikwenda mahakamani kwa ishu ipi. Hata hivyo ninavyojua, FIFA kuna masuala yanayoweza kupelekwa Mahakamani na mengine hayapelekwi. Haiwezekani kwa mfano mtu kaiba halafu unasema FIFA hairuhusu kwenda Mahakamani, sio kweli,” alisema Tandau.

Tandau alisema hajui nakala ya hukumu ya Wambura ikoje, lakini hata likifika FIFA lazima kuna vitu wataangalia, ilikuwaje hadi Wambura akaenda Mahakamani, na kama alikosea lazima watasema na kama alikuwa sahihi pia itajulikana.

Hata hivyo masuala ya soka kupelekwa mahakamani wala sio geni na halijawahi kutokea kwa Wambura pekee.

Mei mwaka huu, Mahakama Kuu nchini Kenya ilitengua uamuzi wa Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini humo (FKF) wa kumfungia aliyekuwa Rais wa Shirikisho hilo, Sam Nyamweya.

Mwaka 2015, Idara ya ujasusi ya Marekani (CIA) vilianzisha uchunguzi kwa aliyekuwa Rais wa FIFA, Sepp Blatter juu ya masuala ya ubadhilifu ambapo baadaye alishtakiwa kwenye Mahakama Kuu nchini Uswizi na kung’oka ndani ya shirikisho hilo.

Advertisement