Yanga ijipange kumkabili Mghana wa Pyramids FC

Thursday October 10 2019

 

By Eliya Solomon

Dar es Salaam. Mshambuliaji John Antwi ni miongoni mwa wachezaji hatari katika kikosi cha Pyramids FC anayepaswa kutazamwa kwa ukaribu na mabeki wa Yanga wakati timu hizo zitakapokutana katika mchezo wa mchujo wa kuwania nafasi ya kucheza makundi ya kombe la Shirikisho Afrika.

Mghana Antwi amefunga mabao matano katika michezo 11 ya mashindano yote msimu huu wa 2019/20, ambao Pyramids FC wanashiriki kwa mara ya kwanza kwenye mashindano ya kimataifa.

Mshambuliaji huyo, alifunga mabao mawili katika mchezo wa awali wa Pyramids FC katika Kombe la Shirikisho dhidi ya Étoile du Congo, Agosti 10 wakati wakiibuka na ushindi wa mabao 4-1.

Mzaliwa huyo wa Takoradi, Ghana alifunga mabao mengine mawili katika mchezo wa Kombe la FA nchini humo dhidi ya Haras El Hodood, Agosti 30, mabao yake mawili, yaliifanya Pyramids FC kusonga mbele kwa hatua iliyofuata.

Licha ya kutokuwa na bao upanda wa Ligi Kuu Misri ndani ya michezo mitatu, Antwi alifunga bao lake la tano msimu huu kwenye kikosi hicho, katika mchezo wa raundi ya kwanza ya kombe la Shirikisho   Afrika, Septemba 29 dhidi ya Belouizdad ya Algeria.

Bao hilo wakiwa ugenini liliipeleka Pyramids FC katika hatua ya mchujo ambapo wamepagwa na Yanga, kutokana na kusonga kwao mbele kwa matokeo ya jumla ya mabao 2-1.

Advertisement

Mbali na nyota huyo, wachezaji wengine hatari kwenye kikosi hicho ni Erick Traore mwenye mabao manne, Mohamed Farouk na Abdallah Said wote wakiwa na mabao matatu kila mmoja huku, Ibrahim Hassan akiwa na mabao mawili katika mashindano yote.

Pyramids FC ilianzishwa 2008 na kucheza madaraja tofauti nchini Misri kabla ya kupanda Ligi Kuu, 2014, ujio wa tajiri, Salem Al Shamsi, uliifanya timu hiyo kuwa na nguvu kubwa kifedha kiasi cha kufanya kazi na aliyekuwa kipa wa zamani wa AC Milan, Mbrazili Dida.

Advertisement