Yanga yaruka mtego hatari Rollers

Thursday August 22 2019

 

By KHATIMU NAHEKA

YANGA imebakiza saa 48 kabla ya kujua hatma yao kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi Tonwship Rollers ya Botswana, lakini ghafla tu Shirikisho la Soka Afrika (CAF) likashusha nyundo moja kwa wenyeji na kuwapa kicheko vijana wa Jangwani.

Walichofanya Caf ni kama kutibua mipango mizima ya wenyeji Township katika mchezo huo wa Jumamosi utakaopigwa kwenye jiji la Gaborone baada ya kubadili uwanja wa mchezo kitendo kilichowatibua mabosi wa wenyeji hao.

Akizungumza na Mwanaspoti kutoka Gaborone Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano ya Yanga Rodgers Gumbo alisema wakiwa katika kikao cha maandalizi ya mchezo huo Caf walituma taarifa ya kubadili uwanja wa mchezo.

Uwanja ambao Yanga walikuwa wanatakiwa kuutumia ni wa kipimo kidogo sawa na ule wa Azam Complex ambao Caf uliukataa kwa kutokidhi viwango.

“Tunaendelea vyema na maandalizi na sasa tumetoka katika kikao (juzi jioni) kujadili mambo mbalimbali, lakini habari nzuri kwetu uwanja ambao wenzetu walitaka kuutumia umezuiwa na Caf,” alisema Gumbo.

Gumbo alisema taarifa hiyo ilionyesha kuwachanganya Township na maafisa wa Shirikisho la soka la Botswan wakionyesha kubadili haraka ajenda za kikao na kuanza kuwasiliana na CAF ambao walishafanya maamuzi yao.

Advertisement

“Ilipokuja taarifa hiyo jamaa zetu hawakufurahi ikionyesha walikuwa wamejipanga kwa mengi katika uwanja huo tunaoambiwa ni mdogo kuliko huu ambao utatumika sasa,”

Bosi huyo alisema habari hiyo ni njema kwao ambapo sasa mchezo huo utachezwa katika uwanja mkuu wa nchini humo ambao hauna tofauti kubwa na ule wa Taifa pale Temeke.

MTANZANIA AWAPA HOTELI

Katika kukwepa hujuma zozote nje ya uwanja, Gumbo alisema timu yao imelazimika kutumia hoteli ya Crystal Palace ambayo inamilikiwa na Mtanzania.

Gumbo alisema bosi wa hoteli hiyo amewaambia kwamba wasiwe na wasiwasi wakiwa hapo kwani hakuna mtu atakayeweza kuwafanyia hujuma yoyote.

“Tutatumia hoteli hiyo, jambo zuri tumekuta inamilikiwa na Mtanzania aliyetuhakikishia mambo mengi, ila nasi tumekubaliana naye katika maisha yetu hapa.”

Yanga inahitaji ushindi au sare yoyote ya kuanzia mabao mawili kusonga mbele baada ya kutoa sare nyumbani ya bao 1-1.

Advertisement