Yanga yasukwa upya, vigogo wote wang’oka

BAADA ya sakarasi nyingi hatimaye mambo yameanza upyaa huko Yanga baada ya mchakato wa mabadiliko makubwa ndani ya klabu hiyo kupewa baraka zote.

Awali, mchakato wa uchaguzi kujaza nafasi zilizowazi ikiwemo ya aliyekuwa Mwenyekiti wa klabu hiyo, Yusuf Manji, uligubikwa na utata mwingi huku baadhi ya wajumbe wakienda kuupinga mahakamani.

Pia, upande wa Yanga ulikuwa ukipinga uchaguzi huo kusimamiwa na Kamati ya Uchaguzi ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), jambo ambalo lilielezwa kuwa ni kinyume cha katiba.

Lakini, jana Mwanaspoti limedokezwa kuwa mchakato wa uchaguzi ndani ya klabu hiyo utachukua sura mpya ndani ya siku chache zijazo, baada ya vigogo wa klabu hiyo kukaa kizito jana Jumatano na kubariki mabadiliko makubwa.

Habari za kuaminika kutoka ndani ya kikao hicho kilichofanyika Makao Makuu ya Yanga, Jangwani, kikiwahusisha Baraza la Wadhamini la klabu hiyo chini ya Mwenyekiti wake George Mkuchika, ambaye ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Utumishi wa Umma na Utawala Bora na baadhi ya wajumbe wa kamati ya utendaji.

Hoja kubwa katika kikao hicho ilikuwa ni mustakabali wa mchakato wa uchaguzi na uongozi wa klabu hiyo ambapo, baada ya hoja ya awali ya kuwataka wajumbe wa kamati ya utendaji waliosalia kujiuzulu, kutokubaliana maamuzi yakaja tofauti.

Uamuzi wa kikao hicho ukawa mchakato huo uanze upya na Yanga ifanye uchaguzi kamili na sio ule wa awali wa kujaza nafasi, ambapo kabla ya mchakato huo uitishwe mkutano mkuu wa dharura.

Mkutano huo wa dharura utakuwa maalum kwa kuwajulisha wanachama wa klabu hiyo juu ya maamuzi hayo na kupanga tarehe mpya ya uchaguzi.

Katika kikao hicho mbali na Mkuchika ambaye pia ni Mbunge wa Newala, wengine waliohudhuria ni Mama Fatma Karume, Jaji Mstaafu John Mkwawa, Mzee Jabir Katundu huku wajumbe wa Kamati ya Utendaji wakiwa Hussein Nyika na Samuel Lukumay.

Kufuatia taarifa hiyo Mwanaspoti lilimtafuta Kaimu Mwenyekiti wa Yanga, Samuel Lukumay mbaye alikiri kufanyika kwa kikao hicho na wameridhia mambo kadhaa.

Alisema mchakato huo sasa utaanza upya ambapo wao wajumbe wa kamati ya utendaji waliosalia watajizulu katika mkutano mkuu utakaoitishwa.

“Tumeona tuchukua maamuzi hayo ya uchaguzi kufanyika upya na uwe ni uchaguzi kamili sio ule wa kujaza nafasi tena kama ilivyokuwa awali,” alisema Lukumay.

“Unajua kama tungefanya huu uchaguzi wa kujaza nafasi ina maana mwakani tena tungekuwa na uchaguzi mwingine, lakini tukumbuke mwakani kutakuwa na uchaguzi wa nchi tumeona tusichanganye mambo.

“Tutaitisha mkutano mkuu baada ya siku chache kuwajulisha wanachama ili na sisi tuliosalia tukajiuzulu na kama kutakuwa na anayetaka kuendelea atagombea.

“Kuhusu tarehe ya uchaguzi na utaanza lini tutatangaza hapo baadaye katika mkutano huo huo wa wanachama ambao, kila kitu kitatangazwa baadaye.”