Yondani, Manula waibua hofu mazoezini

Muktasari:

 

  • Manula ndiye kipa tegemeo wa Taifa Stars kutokana na kiwango chake kama ilivyo kwa Kelvin Yondani ambaye ni mmoja wa mabeki Bora kwenye Ligi Kuu Bara kwa sasa.

Dar es Salaam. Kipa namba moja  wa Taifa Stars, Aishi Manula na beki Kelvin Yondani leo Jumamosi wameshindwa kufanya mazoezi na wenzao hivyo kuzua wasiwasi kama kesho Jumapili watakuwepo katika mchezo dhidi ya Uganda.

Manula hakuwepo kabisa mazoezini wakati Yondani alikudhuria mazoezi hayo lakini alikaa nje ya uwanja akipatiwa matibabu.

Daktari wa Taifa Stars, Richard Yomba amesema Manula ameshinda kufanya mazoezi kwa sababu ameenda hospitali baada ya kushtua mkono.

"Manula ameshtua mkono na unamuuma hivyo amepelekwa hospitali ili kuangaliwa lakini kesho (Jumapili) dhidi ya Uganda naamini atakuwa vizuri na atacheza.

"Yondani alishtua mguu wake wa kulia hivyo ikabidi tumpumzishe mazoezi ili kumpooza na barafu lakini anaendelea vizuri.

Dk Yomba alisema zaidi ya wachezaji hao hakuna mchezaji mwingine aliye majeruhi na wote wako fiti tayari kwa mchezo huo.

Taifa Stars inahitaji kuifunga Uganda huku ikiombea Lesotho afungwe na Cape Verde au mechi hiyo imalizike kwa sare ili ifuzu Afcon.