Zahera, Aussems waibua mjadala kila kona

Thursday February 14 2019

 

By Imani Makongoro, Mwananachi [email protected]

Dar es Salaam. Wakati kocha wa Yanga, Mwinyi Zahera akisema wako tayari kwa matokeo ya aina yoyote siku hiyo, ushindi wa Simba dhidi ya Al Ahly juzi, umetajwa kuwa silaha kubwa ya kuwamaliza watani wao, Jumamosi watakapokutana katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Katika mchezo huo wa hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Al Ahly, Simba iliibuka na ushindi wa bao 1-0 ambao umefanya idadi kubwa ya wadau wa soka kuamini utaiweka sawa kisaikolojia.

Timu hizo zitakutana ikiwa ni mchezo wa pili wa Ligi Kuu, baada ya kutoka suluhu kwenye mechi iliyozikutanisha katika mzunguko wa kwanza msimu huu.

Wadau wa soka walipozungumza na gazeti hili kwa nyakati tofauti jana, walitoa maoni yao ingawa walidai ushindi wa juzi, utaifanya Simba iingie uwanjani ikiwa sawa kisaikolojia kulinganisha na Yanga ambayo hali yao ya kujiamini iko chini.

Hata hivyo, waliweka msisitizo kuwa kitu pekee kinachoweza kubadili upepo na kuibeba Yanga ni mbinu na maandalizi ya Zahera kwa timu ambayo yana umuhimu kwa asilimia 60.

Kauli za wadau

Advertisement

“Kitendo cha kuifunga Al Ahly ambayo ni timu kubwa Afrika, halafu wanakwenda kucheza na Yanga, kwa vyovyote vile lazima Simba itaingia kwenye mechi hiyo ikiwa inajiamini mno,” alisema mchambuzi wa soka nchini Ally Mayay.

Alisema ingawa mechi ya watani wa jadi haitabiriki kutokana na maandalizi ya timu hizo zinapojiandaa kukutana, mashabiki wa Yanga watakwenda uwanjani wakiwa na hofu kulinganisha na Simba.

“Kuanzia ubora wa timu ya Simba, ubora wa mchezaji mmoja mmoja wa Simba na Yanga, Simba wako vizuri. Huwezi kulinganisha kiwango cha Manula (Aishi) na Kabwili (Ramadhani) au Dida (Deogratias Munishi) na Kindoki (Klausi) .

“Achilia mbali wachezaji wengine, Simba wako vizuri. Ili Yanga washinde, lazima kwanza kocha awaandae kisaikolojia wachezaji wake, kwa sababu itakuwa mechi ya wanaocheza mpira na wanaopambana kucheza mpira,” alisema Mayay.

Mwanasaikolojia, Modesta Kimonga wa Chuo cha Elimu Patandi Tawi la Tanga alisema kisaikolojia, Yanga ina hofu na mchezo huo, licha ya kuonyesha ujasiri lakini hawana uhakika wa kushinda kama ilivyo kwa Simba.

“Mbali na hofu, lakini pia wanajiuliza kama Simba wametoka kucheza na Al Ahly na kuifunga itakuwa vipi kwao? Lakini ili hali hiyo isiwakabili wachezaji, ni wakati wa kocha na wasaidizi wake kuiandaa timu kisaikolojia,” alisema Kimonga.

Mwanasaikolojia huyo alisema katika maandalizi wakubaliane na hali halisi katika soka kuna matokeo ya aina tatu kushinda, kufungwa au kutoka sare aina ya aina yoyote.

Hata hivyo, alisema Simba inatakiwa kujiandaa pia, kama iliweza kuifunga Al Ahly hata Yanga licha ya kuonekana dhaifu ina nafasi ya kushinda.

Mchambuzi Alex Kashasha ‘Mwalimu Kashasha’ alisema Simba ina faida kubwa katika mchezo huo hasa baada ya kuifunga Al Ahly.

“Yanga kitakachowafanya wapate matokeo ni mbinu za kocha Zahera, asilimia 60 ushindi wa Yanga uko mikononi mwake na asilimia 40 ndizo za wachezaji,” alisema Mwalimu Kashasha.

“Mechi ya watani haitabiriki, lakini kwa mechi ya Jumamosi, Simba ina nafasi kubwa zaidi ya Yanga ambayo ili kupata matokeo itategemea na mpango wa kiufundi wa kocha,” alisema Kashasha.

Mwalimu Kashasha alisema katika mechi hiyo ni jukumu la kocha kuwaandaa kisaikolojia wachezaji wake ili wakathibitishe ubora wao na kutengeneza majina mbele ya Simba yenye wachezaji bora na ghali.

Hata hivyo kwa upande wake kocha Zahera amesisitiza katika mchezo huo wako tayari kwa matokeo ya aina yoyote yale Jumamosi.

“Sisi hatuna presha na hiyo mechi, labda upande wa pili ndiyo wana presha, tunaendelea na mazoezi na leo (jana) tumefanya mazoezi ya mbinu na ufundi na kesho (leo) tutaendelea na maazoezi ya kupata muunganiko bora kwenye timu yangu,” alisema Zahera.

Kocha huyo alibainisha kwamba mpira si hesabu, kwamba moja jumlisha moja utapata mbili, hivyo matokeo ya Simba ya juzi wala si kitu kwao kuelekea kwenye mechi ya Jumamosi.

“Siku hazifanani, ndivyo mpira nao ulivyo, kushinda jana (juzi) sio sababu kuwa watatufunga. Tulianza ligi pamoja kila mmoja akisaka ubingwa, hivyo hatuna sababu ya kuwa na presha.

“Tukishinda nitafurahi lakini hata tukitoka sare au tumefungwa hakuna kitakachobadilika,” alisema kocha huyo raia wa DR Congo.

Simba inaingia kwenye mchezo huo ikiwa na rekodi nzuri ya kupoteza mechi saba mfululizo dhidi ya Yanga pindi walipokutana kwenye mashindano mbalimbali.

Katika mechi hizo saba, Simba wameshinda mechi nne ambapo mbili ni za Ligi Kuu, moja Kombe la Mapinduzi na moja ya Ngao ya Jamii huku zilizobaki tatu za ligi wakitoka sare.

Advertisement