Zidane ampandia dau Kante

Madrid, Hispania. Real Madrid imeanza kumtolea macho kiungo wa Chelsea, N’Golo Kante baada ya kuweka mezani Pauni86 milioni ikimtaka katika dirisha dogo.

Mbali na kuweka fedha hizo, Real Madrid itamtoa mshambuliaji James Rodriguez kama njia ya kupata saini ya Kante.

Kocha wa Real Madrid, Zinedine Zidane amekuwa na ndoto ya kumsajili mchezaji huyo wa kimataifa wa Ufaransa.

Real Madrid tayari imemsajili Eden Hazard akitokea Chelsea katika majira ya kiangazi msimu uliopita akitua Santiago Bernabeu kwa dau la Pauni 150 milioni.

Kante anatajwa kuwa mmoja wa wachezaji bora wa kiungo barani Ulaya na amekuwa akiwindwa na klabu mbalimbali.

Rodriguez amesahaulika Real Madrid tangu alipotolewa kwa mkopo kwa misimu miwili akacheza kwa kigogo cha soka Ujerumani, Bayern Munich.

Taarifa za ndani zilidai Chelsea ilitaka kumsajili Rodriguez kabla ya nyota huyo wa kimataifa wa Colombia kupelekwa Bayern Munich.

Real Madrid inataka kutumia nafasi hiyo kupata saini ya Kante ambaye amekuwa na uwezo mkubwa wa kucheza katika nafasi ya kiungo.