#WC2018: Usiyoyajua Kombe la Dunia

Tuesday July 17 2018

Kiungo wa Croatia Luka Modric (kushoto),

Kiungo wa Croatia Luka Modric (kushoto), akiwania mpira na mshambuliaji wa Ufaransa, Antoine Griezmann katika mchezo wa fainali Kombe la Dunia uliochezwa juzi Uwanja wa Luzhniki, Russia.Picha na AFP 

1. Ilichukua takribani dakika 25 tangu kumalizika kwa mechi ya fainali ya 21 ya Kombe la Dunia, hadi kukamilika uandaaji wa jukwaa la kutolea zawadi kwa washindi.

2. Nahodha wa zamani wa Ujerumani, Philipp Lahm, ndiye aliyepewa heshima ya kubeba Kombe la Dunia kutoka chumba lilikohifadhiwa hadi kufikisha uwanjani.

3. Marais watatu walipewa heshima ya kusimama jukwaa kuu wakati wa utoaji tuzo za washindi wa fainali za 21 za Kombe la Dunia, Vladimir Putin (Russia), Emmanuel Macron (Ufaransa) na Kolinda Grabar (Croatia).

4. Kocha wa Ufaransa, Didier Deschamps amekuwa Kocha wa tatu kutwaa Kombe la Dunia, baada ya kutwaa akiwa mchezaji akiungana na Mario Zagallo (Brazil) na Franz Beckenbauer (Ujerumani).

5. Mario Mandzukic amekuwa mchezaji wa kwanza kujifunga katika mechi ya fainali ya Kombe la Dunia tangu kuanzishwa mwaka 1930.

6. Kylian Mbappe (miaka 19 na siku 207) amekuwa mchezaji wa pili mdogo zaidi kuwahi kufunga bao katika mechi ya fainali, Pele wa Brazil, ndiye alikuwa wa kwanza mwaka 1958 alipokuwa na miaka 17 na siku 249.

7. Antoine Griezmann amefikisha mabao 10, katika mashindano makubwa anashika nafasi ya nne kwa wachezaji walioifungia Ufaransa mabao mengi, Michel Platini (14), Just Fontaine (13) na Thierry Henry (12).

8. Ivan Perisic ni mchezaji wa kwanza wa Croatia kufunga na kutengeneza mabao 11 akifunga saba na kutengeneza manne.

9. Pia Perisic amekuwa mchezaji wa pili katika historia ya Kombe la Dunia, kusababisha penalti inayosababisha wafungwe na alipata bao la kusawazisha.

10. Paul Pogba ni mchezaji wa kwanza wa Manchester United kufunga bao katika mchezo wa fainali ya Kombe la Dunia.

Pia Pogba amekuwa mchezaji wa kwanza wa Ligi Kuu England kufunga bao tangu Mfaransa mwenzake Emmanuel Petit alipofunga mwaka 1998.

11. Paul Pogba, amekuwa mchezaji wa kwanza kufunga bao kutoka nje ya ‘boksi’, tangu alipofanya hivyo Marco Tardelli wa Italia dhidi ya Ujerumani mwaka 1982.

12. Mario Mandzukic, amekuwa mchezaji wa pili katika historia ya fainali za Kombe la Dunia kujifunga bao na kuifungia timu yake bao, tangu kocha wa zamani wa Yanga, Mholanzi Ernest Brandts alipofanya hivyo dhidi ya Italia 1978.

13. Mario Mandzukic ni mchezaji wa tano kufunga bao katika mechi ya fainali ya Kombe la Dunia, Kombe la Ulaya na Ligi ya Mabingwa Ulaya, Juventus ‘Kibibi Kizee’ ilipocheza na Real Madrid.

Advertisement