#WC2018: Keane ampa Pogba ruksa kucheza dansi

Muktasari:

Keane alitoa kauli hiyo muda mfupi baada ya Pogba kuisaidia Ufaransa kutwaa ubingwa wa Kombe la Dunia kwa kuilaza Croatia mabao 4-2, katika mchezo wa fainali uliochezwa kwenye Uwanja wa Luzhniki, Russia.

Moscow, Russia. Roy Keane amesema Paul Pogba ana haki ya kucheza dansi kadri anavyotaka kwa kuwa kiwango chake katika mchezo wa fainali ya Kombe la Dunia kilikuwa cha aina yake juzi.

Keane alitoa kauli hiyo muda mfupi baada ya Pogba kuisaidia Ufaransa kutwaa ubingwa wa Kombe la Dunia kwa kuilaza Croatia mabao 4-2, katika mchezo wa fainali uliochezwa kwenye Uwanja wa Luzhniki, Russia.

Kiungo huyo wa Manchester United, alifunga bao la tatu kwa kiki kali ya mguu wa kushoto na alikuwa mchezaji bora wa mchezo huo baada ya kucheza kwa kiwango bora.

Pogba awaziba mdomo wabaya wake akiwemo kocha Jose Mourinho ambao wamekuwa wakiponda kiwango chake na kudai nyota huyo ni hodari wa kucheza dansi na kuweka nywele dawa.

“Sijali kama Pogba atacheza dansi leo. Anastahili kusakata muziki kwa sababu ni bingwa wa dunia, anaweza kufanya jambo lolote lile,” alisema nguli huyo.

Keane aliyekuwa mchambuzi wa mchezo huo, alisema mchezaji huyo alionyesha kipaji cha soka licha ya mara kwa mara kukumbwa na matukio binafsi nje ya uwanja.

Nahodha huyo wa zamani wa Man United alisema anashangaa kocha wa Ufaransa Didier Deschaps kumtumia vyema Pogba, lakini Mourinho amekwaa kisiki mara kadhaa.

Naye Rio Ferdinand aliyewahi kuwika Man United, alidokeza kuwa Pogba alionyesha nidhamu katika eneo la ulinzi na ushambuliaji.

Nguli huyo wa zamani wa England, alisema Ufaransa inastahili kuwa mabingwa wa dunia, baada ya kucheza kwa kiwango bora fainali hizo.

Ufaransa imeweka historia ya kutwaa ubingwa wa Kombe la Dunia mara mbili mwaka 1998, 2018 na Deschamps ameweka rekodi ya kutwaa taji hilo akiwa mchezaji wa timu hiyo na kocha.