#WC2018: Ufaransa, Croatia somo tosha Stars

Tuesday July 17 2018

 

By Charles Abel, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Wadau wa soka Tanzania wanaamini uwekezaji katika soka la vijana ndiyo siri ya Ufaransa kutwaa ubingwa wa Kombe la Dunia kwa kuifunga Croatia mabao 4-2 kwenye mchezo wa fainali uliochezwa Moscow, Russia.

Takwimu za fainali hizo zinaonyesha kati ya timu nne zilizofuzu hatua ya nusu fainali, hakuna ambayo wastani wa umri wa wachezaji wake unavuka miaka 28.

Wastani wa umri kwa kikosi cha Ufaransa kilichotwaa ubingwa ni miaka 26 na Croatia iliyoshika nafasi ya pili miaka 27.9.

Ubelgiji iliyoshika nafasi ya tatu ina wastani wa miaka 27.6 na England iliyomaliza katika nafasi ya nne ni miaka 26.

Pamoja na idadi kubwa ya vikosi vya timu kujumuisha kundi kubwa la wachezaji wenye umri mdogo, mambo mengine yaliyosisimua kwenye fainali hizo na kuteka hisia za watu nchini ni matumizi ya teknolojia ya video ya kuwasaidia waamuzi (VAR).

Wadau wa soka nchini wanaamini jambo kubwa linapaswa kuigwa na kufanyia kazi kwa haraka ni kuweka mipango endelevu katika soka la vijana wakidai ndio njia pekee inayoweza kuiweka Tanzania kwenye ramani ya kimataifa.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti, wadau wa soka walisema Ufaransa iliyotwaa ubingwa na nchi nyingi zilizofanya vizuri kwenye fainali hizo zina msingi imara wa soka la vijana ambao kama utapewa kipaumbele hapa nchini utasaidia kuhitimisha ndoto ya muda mrefu ya Tanzania kushiriki mashindano makubwa likiwemo Kombe la Dunia na Mataifa Afrika.

“Mpira wa miguu ni sayansi na maandalizi ya timu zetu kabla ya kushiriki mashindano mbalimbali ni lazima yaandaliwe kisayansi ili kupata kile tunachohitaji na maandalizi hayo ni lazima yafanyike kwa kuangalia wenzetu waliofanikiwa.

“Kama nchi lazima tutengeneze mazingira sahihi ya kushindana kwanza kwenye ngazi ya bara letu na baada ya hapo tuanze kupiga hesabu za Kombe la Dunia.

Msingi wa maandalizi lazima uanzie kwa vijana ambao watatengenezwa na kuandaliwa vizuri kwa njia sahihi kama wenzetu waliopiga hatua walivyofanya,” alisema Kaimu Mkurugenzi wa Ufundi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Oscar Milambo.

Kiungo wa zamani wa Yanga na Taifa Stars, Aaron Nyanda alisema kupitia Fainali za Kombe la Dunia, thamani ya soka la vijana imejidhihirisha kama njia kuu ya mafanikio.

“Mashindano ya mwaka huu yameonyesha kwamba hakuna jambo linaloshindikana kwenye mpira wa miguu. Timu ambazo hazikutarajiwa kufanya vizuri zilifika hatua za juu zaidi kuliko zile ambazo zilipewa nafasi. Hii inamaanisha zilijiandaa vizuri muda mrefu hadi zikaweza kupata mafanikio hayo.

“Kama nchi, nadhani tunapaswa kujipanga upya katika namna ambayo tunasaka vipaji vyetu vya soka na uendelezaji wake. Tuwekeze kwa wachezaji wetu hasa wenye umri mdogo wanaweza kwenda kwa wingi nje ya nchi kucheza soka la kulipwa,”alisema Nyanda.

Advertisement