Mbowe ahoji bungeni ujenzi Daraja la Wami, Serikali yamjibu

Naibu Waziri wa Ujenzi,Uchukuzi na Mawasiliano Eliasi Kwandikwa akijibu maswali ya wabunge wakati wa kipindi cha maswali na majibu bungeni jijini Dodoma leo. Picha na Ericky Boniphace

Muktasari:

  • Serikali imesaini mkataba wa kujenga daraja jipya katika eneo la Mto Wami mkoani Pwani ili kupunguza ajali ambazo zimekuwa zikitokea mara kwa mara katika eneo hilo na kurahisisha usafiri kwa mikoa ya Kaskazini

Dodoma. Serikali imeanza kujenga daraja jipya eneo la Wami mkoani Pwani ili kuzuia ajali ambazo zimekuwa zikitokea mara kwa mara.

Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Eliasi Kwandikwa ameliambia Bunge leo Ijumaa  Novemba 9, 2018 kuwa mkandarasi Power Construction Corporation kutoka China amekwisha saini mkataba toka Juni 28, 2018.

Kwandika ametoa kauli hiyo wakati akijibu swali la mbunge wa Hai (Chadema), Freeman Mbowe ambaye hakuwepo na swali hilo liliulizwa kwa niaba yake na Mbunge wa Rombo (Chadema), Joseph Selasini.

Mbowe ametaka kujua Daraja la Wami lilijengwa mwaka gani na kama Serikali haioni ajali zilizotokea hapo zinatokana na wembamba wa daraja na kuna mpango wa kupanua daraja hili sambamba na eneo lote la barabara la mteremko wa mto huo.

"Daraja la Wami lenye urefu wa mita 88.75 lililoko mkoa wa Pwani lilijengwa mwaka 1959 na ndicho kiungo cha kutoka Chalinze kwenda ukanda wa Kaskazini," amesema Kwandikwa

Amesema daraja hilo jipya litakuwa na urefu wa mita 513.5 na upana wa mita 11.85 na litajengwa umbali wa mita 670 pembeni mwa daraja la zamani.

Kwa mujibu wa Naibu Waziri, kazi ya ujenzi wa daraja hilo utakuwa wa miezi 24 na litagharimu Sh67.8 bilioni.