Makambo azua hofu Yanga kuishusha daraja Ruvu Shooting

Tuesday May 14 2019

 

By ELIYA SOLOMON

MAAFANDE wa Ruvu Shooting, watakuwa na kibarua kizito leo kumzuia mshambuliaji wa Yanga, Heritier Makambo kwenye mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara ‘TPL’.

Makambo ambaye amekuwa akitegemewa kwenye safu ya ushambuliaji ya Yanga, yupo kwenye kinyang’anyiro cha kuwania kuwa mfungaji bora wa TPL , akiwa na mabao 16.

Katika mchezo uliopita ambao ulichezwa uwanja wa taifa baina ya timu hizo mbili  jijini Dar es Salaam, Disemba 16 mwaka jana, Makambo aliizamisha Ruvu Shooting kwa kuifungia Yanga bao la ushindi kwenye matokeo ya mabao 3-2.

Makambo amezidiwa mabao manne na Meddie Kagere (20)  wa Simba ambaye anaongoza orodha ya washambuliaji wanaowania kiatu cha ufungaji bora Ligi Kuu Tanzania Bara.

Mbali na vita hiyo ya Makambo, Yanga ambao wapo nafasi ya pili kwenye msimamo wakiwa na pointi 80,  wanahitaji ushindi kwenye mchezo wa leo ili kuweka hai matumaini ya kutwaa ubingwa wa Ligi hiyo ambayo inaelekea ukingoni.

Ruvu Shooting ambao wanachangamoto kwenye safu yao ya ulinzi ambayo inaruhusu mabao 40 msimu huu, nao wanahitaji ushindi kwenye mchezo  huo ili kutokuwa kwenye hatari ya kushuka daraja.

Advertisement