Rekodi ya Kagere Simba tishio

Muktasari:

  • Bao la kichwa dhidi ya watani wao Yanga liliifanya Simba ivune pointi tatu katika mechi hiyo ya mzunguko wa pili ambayo ilishinda 1-0.

Dar es Salaam. Wakati Simba ikiendelea kusherehekea ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu, mchezaji nyota Meddie Kagere ni miongoni mwa waliotoa mchango mkubwa kwa timu hiyo hadi ikafanikiwa kutetea taji lake.

Mshambuliaji huyo amechangia zaidi ya robo ya pointi zote 91 kutokana na mabao aliyofunga ambazo zimeiwezesha Simba kutwaa ubingwa huku ikiwa na mechi mbili mkononi dhidi ya Biashara United na Mtibwa Sugar.

Kagere aliyesajiliwa na Simba mwanzoni mwa msimu huu akitokea Gor Mahia ya Kenya, ameipatia Simba pointi 22 sawa na asilimia 25.28 ya pointi zote kutokana na mabao yake katika mechi nane ambazo pengine kama asingefunga, timu hiyo isingeweza kuvuna pointi katika michezo husika

Na hilo lingewafanya hata ubingwa wasipate kwa kuwa kama Simba isingepata pointi hizo, hadi sasa ingekuwa na 69 ambazo zingewafanya kuwa nyuma ya Azam FC inayoshika nafasi ya tatu kwa pointi 72.

Kagere aliipa Simba pointi tatu alipofunga bao moja katika ushindi 1-0 dhidi ya Prisons kwenye mzunguko wa kwanza, akaipa tena pointi hizo kwa kuifungia mabao mawili iliposhinda 2-0 dhidi ya Mbeya City na mechi nyingine aliyoipa pointi tatu ni ile waliyocheza na JKT Tanzania Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga iliposhinda 2-0, ambayo yote yalifungwa na nyota huyo.

Bao la kichwa dhidi ya watani wao Yanga liliifanya Simba ivune pointi tatu katika mechi hiyo ya mzunguko wa pili ambayo ilishinda 1-0.

Katika ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Coastal Union ugenini Tanga, Kagere alipachika yote kama alivyofanya dhidi ya Ndanda wiki iliyopita ambapo alifunga idadi kama hiyo katika ushindi wa mabao 2-0.

Pia kama siyo Kagere, Simba ingepoteza pointi mbili dhidi ya Azam kwani kama mabao yake mawili asingeyafunga, mechi hiyo ingemalizika kwa sare ya bao 1-1. Simba ilishinda 3-1.

Ni Kagere tena aliwapatia Simba pointi mbili za ziada katika mechi ya ugenini dhidi ya Mbeya City waliposhinda mabao 2-1 kupitia bao lake moja alilopachika kwani vinginevyo, mechi hiyo ingemalizika kwa sare ya bao 1-1.

Kati ya timu 20 zinazoshiriki Ligi Kuu msimu huu, 12 zimeonja ladha ya mabao ya Kagere, nyingine akizifunga katika mechi zote mbili za msimu nyumbani na ugenini huku nyingine akizifunga mara moja ingawa ameshindwa kufua dafu mbele ya timu saba ambazo hakuzifunga.

Timu 12 zilizofungwa na Kagere ni Lipuli, Yanga, Prisons, Singida United, Mbao, Mwadui, Ruvu Shooting, Azam, Ndanda, JKT Tanzania, Mbeya City na Coastal Union ilhali saba ambazo hakuzifunga ni Kagera Sugar, Alliance, KMC, Stand United, African Lyon, Biashara United na Mtibwa Sugar.

Coastal Union ndiyo timu ambayo imeonja makali zaidi ya Kagere kwani amefunga mabao matano dhidi ya timu hiyo ikifuatiwa na Mbeya City aliyoifunga mara tatu wakati timu za Mwadui, Ruvu Shooting, Azam, Ndanda na JKT Tanzania kila moja imeruhusu nyavu zake kutikiswa mara mbili na mshambuliaji huyo.

Nyavu za Uwanja wa Taifa ndizo zinaongoza kutikiswa zaidi na Kagere kwani amefunga mabao tisa kwenye uwanja huo ukifuatiwa na Uhuru ambao amepachika matano. Mwingine ni Mkwakwani (manne) na viwanja vya Sokoine Mbeya, Kambarage (Shinyanga), Namfua (Singida) na Samora - Iringa, kila mmoja amepachika bao moja. Kagere ni hatari dakika 15 za mwanzo za mchezo kwa kuwa muda huo amefunga mabao saba kati ya 23. Mabao mawili amefunga dakika ya 16 hadi ya 30 na kuanzia ile ya 31 hadi ya 45 pia amefunga mawili.

Katika kila dakika 15 za kipindi cha pili amefunga manne manne, jambo linalomfanya awe amefunga idadi kubwa zaidi ya mabao kipindi cha pili ambayo ni 12 na cha kwanza 11.

Katika hali ya kushangaza, kati ya mabao 23, matatu amefunga dakika ya 11 katika mechi tatu tofauti ambazo ni dhidi ya Mbeya City Uwanja wa Taifa na JKT Tanzania, pia dhidi ya Ndanda FC kwenye Uwanja wa Uhuru.

Katika mechi 36 ambazo Simba imecheza hadi sasa, raia huyo wa Rwanda amecheza michezo 31 ambayo ni sawa na asilimia 86.11 ya mechi zote ambazo Simba imecheza kwenye Ligi Kuu msimu huu.

Ni mechi nne tu ambazo amekosa dhidi ya Alliance FC, Singida United, African Lyon na KMC.

Asemacho Kagere, Aussems

Akizungumzia mafanikio yake, Kagere alisema siri pekee ni kujituma, kuweka malengo na ushirikiano kutoka kwa wenzake na kwamba huwa hachagui mechi kubwa au ndogo lengo likiwa ni kuipa ushindi timu yake ya Simba.

Kocha wa Simba, Patrick Aussems alisema kuwa kinachofanywa na mchezaji huyo ni ishara tosha ya ubora wa kikosi chake katika mashindano ya msimu huu.