Mayanja hana presha na kina Niyonzima

Kocha wa KMC, Jackson Mayanja amesema hana presha na mechi yao ya kesho dhidi ya AS Kigali ya Rwanda akidai wamepania kuifunga ikiwa kwao ili kujitengenezea mazingira rahisi katika mchezo wa marudiano.
KMC tayari ipo Kigali tangu jana na imekuwa ikijifua kwa mara ya mwisho kabla ya kuwakabili wenyeji wao hao ambao wana nyota wa kimataifa wa zamani wa Simba na Yanga, Haruna Niyonzima katika mechi ya raundi ya awali ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Mechi hiyo itapigwa kwenye Uwanja wa Amahoro, mjini Kigali na Kocha Mayanja anaamini kama watapata ushindi katika mchezo huo basi hawatakuwa na kazi kubwa katika mchezo wa marudiano utakaofanyika Agosti 23.
"Mechi itakuwa ngumu sana kwa sababu tutakuwa ugenini lakini hiyo haitufanyi kuogopa kwani lazima tupambane kuweza kupata matokeo mazuri. Kikubwa kilicho kwenye malengo yetu ni kuhakikisha hiyo mechi tunashinda  kwani ukishinda ugenini  unakuwa  huna kazi kubwa ya kusaka ushindi nyumbani," alisema Mayanja.
Mayanja aliyewahi kuzinoa Kagera Sugar, Coastal Union na Simba kwa hapa nchini alisema naamini wachezaji waozefu kama kipa Juma Kaseja, Besala Bokungu   wataibeba timu katika mchezo huo wakishirikiana na chipukizi.
KMC inashiriki michuano hiyo kwa mara ya kwanza baada ya kumaliza nafasi ya nne katika Ligi Kuu msimu uliopita na kupata bahati hiyo kufuatia kuongezwa kwa idadi ya timu wawakilishi wa Tanzania na hasa baada ya Azam waliomaliza nafasi ya tatu kubeba pia Kombe la FA.
Wawakilishi wengine msimu huu ni Azam wanaocheza Kombe la Shirikisho pia, Simba na Yanga zitakazotupa karata zao kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu.