Man United yaichapa Chelsea 4-0

Manchester, England
NDANI ya dakika 15 za kwanza ilionekana kama Manchester United ya Ole Gunner Solskjaer inakwenda kupoteza mchezo wake wa kwanza wa Ligi Kuu ya England, ambapo ilizidiwa kila idara. Chelsea ikiongozwa na Pedro Rodriguez, Tammy Abrham na Emerson ilisukuma mashambulizi makali langoni mwa Man United.
Katika mashambulizi hayo ya Chelsea, mara mbili washambuliaji wake waligogesha mwamba wa goli huku mashuti mengine yakienda nje. Hata hivyo, dakika ya 18 shambulizi la Man United liliishia kuzalisha penalti baada ya beki wa Chelsea, Kort Zouma kumkwatua Marcus Rashford ndani ya eneo la hatari na mwamuzi Anthony Taylor kuamuru upigwe mkwaju wa penati.
Rashford akitumia ufundi mwingi alifunga penati hiyo na kuitanguliza Man United kwa bao 1-0 ambalo lilidumu hadi kipindi cha kwanza kinamalizika. Licha ya kwenda mapumziko ikiwa nyuma, lakini Chelsea ilimililki mchezo huo kwa muda wote wa dakika 45.
Kipindi cha pili, Man United iliingia uwanjani ikiwa na shauku ya kupata mabao mengine zaidi ambapo, Rashford na Anthony Martial waliongoza mashambulizi huku Pogba akisimama eneo la katikati akishrikiana na Andres Perreira wakati safu ya ulinzi ilikuwa chini ya beki mpya wa kati, Harry Maguire akicheza sambamba na Wan Bissaka, Victor Linderlof na Luke Shaw walimfanya Dea Gea kuwa salama muda wote.
Katika mchezo huo, Man United iliandika bao la pili dakika ya 65 kupitia kwa Martial akiunganisha krosi ya Perreira kabla ya Rashford tena kupachika bao la tatu. Iliwachukua Man United sekunde 95 tu kufunga mabao mawili la pili na la tatu.
Kama vile ikionekana kuwa matokeo yanakwenda kubaki 3-0, dakika ya 82 ya mchezo kinda mpya wa Man United, Daniel James aliyeingia kuchukua nafasi ya Perreira alipigilia msumari wa mwisho kwa kupachika bao 4-0 akitumia vyema pasi ya Pogba, ambaye kwenye mchezo huo alipiga pasi mbili za mabao.
Takwimu za mwisho wa mchezo zimeonyesha kwamba, Chelsea ilikuwa na umiliki wa mpira kwa asilimia 53.8 dhidi ya 46.2 za Man United huku ikipiga mashuti 18 na saba kati ya hayo ndio yalilenga lango wakati kwa upande wa wapinzani wao, walipiga mashuti 11 huku matano yakilenga goli.
Chelsea ilipata kona tano dhidi ya tatu za Man United.

VIKOSI:
Manchester United: De Gea; Wan-Bissaka, Maguire, Lindelof, Shaw; McTominay, Pogba; Pereira (James), Lingard (Mata), Martial; Rashford (Greenwood)
Chelsea: Arrizabalaga; Azpilicueta, Christensen, Zouma, Emerson Palmieri; Jorginho, Kovacic (Kante); Pedro, Barkley (Pulisic), Mount; Abraham (Giroud).