Neymar, Icardi, Eriksen watikisa usajili Ulaya

Muktasari:

Wachezaji hao wanahusishwa na kutaka kuziahama klabu zao msimu huu kabla ya kufungwa wa dirisha la usajili Agosti 31.

Dirisha la usajili limefungwa England, lakini mataifa mengine barani Ulaya bado heka heka za usajili zinaendelea ikiwemo Italia, Hispania na Ujerumani.

Majira haya ya usajili wa kiangazi kuna matukio mengi ambayo yanaendelea, ikiwemo lile linalomhusisha nyota wa kimataifa wa Brazil, Neymar ambaye analazimisha kutaka kuondoka PSG.

Neymar amekuwa akifanya vituko vya hapa na pale kwenye klabu yake ya PSG yote hiyo ni kuhitaji kwake kurejea Hispania, tayari miamba ya soka nchini humo, Barcelona na Real Madrid wameonyesha nia ya kumsajili.

Pia, yupo Mauro Icardi anahitaji kuondoka   Inter Milan baada ya kutua kwenye klabu hiyo, Romelu Lukaku ambaye tayari amekabidhi jezi aliyokuwa akiitumia ya namba tisa mgongoni.

Mshambuliaji huyo anahusishwa kujiunga na Juventus. Donny van de Beek wa Ajax anatajwa kuwa kwenye rada za Real Madrid, wachezaji wengine wanaoweza kuzihama klabu zao ni Paulo Dybala wa Juventus kwenda Paris Saint-Germain.

James Rodriguez wa Real Madrid kwenda Atletico Madrid, Ivan Rakitic wa Barcelona kwenda Inter Milan, Philippe Coutinho wa Barcelona kwenda Bayern Munich au Paris Saint-Germain.

Christian Eriksen wa Tottenham kwenda Real Madrid au Atletico Madrid, Hirving Lozano wa PSV kwenda Napoli, Ivan Perisic wa Inter Milan kwenda Bayern Munich.